‘Fanyeni utafiti kupata ufumbuzi elimu ya juu’

VYUO  Vikuu nchini vimetakiwa kufanya tafiti, zikiwemo za namna ambavyo elimu ya juu itakidhi matakwa ya sasa ya jamii ya Watanzania.

Agizo hilo limetolewa leo Oktoba 19, 2022 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael, wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na miaka 17 ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Amesema ni vizuri kufanya uchunguzi wa kina, kuhusu mwelekeo wa sasa wa kitaifa na kimataifa na kisha kutafakari ni namna gani vyuo vikuu  vitawawezesha wahitimu kuendana na mwelekeo huo.

“Kama mnavyofahamu, kumekuwa na mjadala kuhusu uwezo wa kujiajiri miongoni mwa wahitimu wa vyuo vikuu, mjadala ambao kwa namna moja au nyingine umezua maswali kuhusu mitaala ya elimu nchini,” amesema Dk Michael na kuongeza:

“Kutokana na mjadala huu, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia umuhimu wa kuipitia upya mitaala, ili iendane na matakwa ya ulimwengu wa sasa, ikiwemo uwezo wa wahitimu kujiajiri na kuwa wabunifu,” amesema.

Amesema wahitimu wengi wapo mtaani, wakisubiri kuajiriwa na hata wengine wamekuwa hawana uelewa wa kujiajiri, lakini kama chuo kikitengeneza mikakati ambayo itaweza kumsaidia mhitimu kujiajiri, basi vijana wengi watapata ajira.

Amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa elimu ya juu kwenye maendeleo ya taifa,  na ongezeko la bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, ni moja tu ya mifano michache ya nia njema ya serikali ya kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu.

Dk Michael amesema kongamano hilo ni muhimu kutafakari ni kwa vipi  DUCE inachangia katika jitihada hizo.

Amesema kama ilivyo kwenye vyuo vingine, serikali kupitia Wizara ya Elimu, itaendelea kutoa ushirikiano kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam katika dhamira yake ya kuendelea kutoa walimu bora, ambao wanahitajika, ili kufikia lengo la kutoa elimu bora kwa Watanzania wote.

Kwa upande wake, Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam, Prof. Stephen Maluka, amesema chuo hicho katika kipindi cha miaka 17 tangu kuanzishwa kwake kimepata mafanikio makubwa.

Alitaja mafanikio hayo ni kuongezeka kwa wahitimu kutoka 522 Mwaka 2008 hadi kufikia 16,330 mwaka 2021, programu kutoka digirii za awali nne hadi tano.

Prof Maluka ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kukisaidia chuo kusomesha baadhi ya watumishi wa chuo, ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya chuo kupitia miradi yake mbalimbali na kutatua changamoto ya miundombinu katika chuo hicho.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button