Festo Kiswaga ajitosa ubunge Isimani

IRINGA: ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga, leo Juni 29, 2025, amechukua rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kugombea ubunge wa Jimbo la Isimani, mkoani Iringa.
Kiswaga ambaye pia aliwahi kuhudumu kama Mkuu wa Wilaya mbalimbali na baadae Kahama na Monduli, amesema amejiandaa kwa moyo, akili na maarifa kuwatumikia wananchi wa Isimani endapo atateuliwa na chama chake na baadaye kushinda uchaguzi huo.
“Uzoefu wangu katika nafasi mbalimbali za kiuongozi serikalini na ndani ya chama umenijenga na kunipa uelewa wa kina juu ya changamoto za wananchi. Ninaamini nina uwezo wa kushirikiana nao kuzitatua na kuharakisha maendeleo endelevu,” alisema Kiswaga mara baada ya kuchukua fomu.

Akizungumzia mwamko wa maendeleo unaoendelea nchini, Kiswaga alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake mahiri na kusisitiza kuwa jitihada zake zinahitaji kuungwa mkono kwa nguvu mpya.
Pia ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanamchagua kwa kishindo Rais Samia na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ili kuendeleza ajenda ya maendeleo ya taifa.
Jimbo la Isimani limeongozwa kwa zaidi ya miaka 30 na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, ambaye pia alikuwa Mbunge wake kwa muda mrefu, na hivyo Kiswaga ameahidi kujifunza kutoka kwa waliomtangulia huku akiahidi kasi mpya ya maendeleo.
“Niko tayari kujifunza kutoka kwa waliotangulia, lakini pia kuleta uongozi unaosikiliza, kushirikisha na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya jimbo letu,” alisisitiza.
Kiswaga ameeleza kuwa Jimbo la Isimani halina sababu ya kubaki nyuma kimaendeleo kwani limebarikiwa kuwa na fursa nyingi za kiuchumi.
Alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni: Kilimo na Ufugaji akisema Isimani ni eneo linalofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara kama mahindi, mpunga, alizeti na mbaazi, pamoja na ufugaji wa kisasa wa ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Aidha alisema baadhi ya maeneo ya jimbo hilo yana utajiri wa madini ambayo bado hayajachimbwa kwa kiwango cha kibiashara, hivyo kuwa fursa ya kuibua ajira na mapato mapya kwa wananchi.
Alizungumzia pia uvuvi akisema maeneo ya bonde la Mtera na vijiji vinavyopakana na mito na mabwawa yanatoa fursa nzuri za uvuvi wa samaki na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba au mabwawa ya kisasa.
Amesema anayo mikakati madhubuti ya kusaidia vijana na wanawake kunufaika na rasilimali hizo kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha, kuwajengea uwezo na kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kwa tija.

