FITI watakiwa kutangaza bidhaa zao

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana amekielekeza Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) kujitangaza kwa lengo la kuuza bidhaa za misitu zinazozalishwa na chuo hicho.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 15,2024 alipozungumza na Menejimenti ya chuo wakati wa ziara ya kikazi katika chuo hicho kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Advertisement

“Tuendelee na mashirikiano kati yetu na vyuo vingine vilivyopo hapa nchini na tujitangaze ili soko la bidhaa zinazotokana na mazao ya misitu, ziuzike hasa kwenye taasisi za Serikali,” amesema Chana.

Aidha, ameielekeza Menejimenti hiyo kuhakikisha mapato ya chuo yanaongezeka ili kiweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

SOMA: Dk Chana aonya wawekezaji wasioendeleza maeneo

Aidha, amekielekeza chuo hicho kutoa mafunzo ya utengenezaji mizinga ya nyuki kwa wananchi ili waweze kufuga asali na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

SOMA: Chana aelekeza Halmashauri kudhibiti moto misitu

Naye, Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi, Dk Zacharia Lupala amesema chuo hicho kimejikita katika kutoa maarifa, ujuzi na huduma ya ugani katika matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na hifadhi za mazingira.

Chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1976 kinatoa mafunzo ya umahiri ya cheti na Diploma ya Viwanda vya Misitu, mafunzo ya muda mfupi ya Viwanda vya Misitu na huduma ya ugani,ushauri na Utafiti wa Viwanda vya Misitu na matumizi endelevu ya mazao ya misitu na hifadhi za mazingira.