Fundi ‘aluminium’ asiyeona, msomi wa PhD

Aduwaza wengi kwa ujuvi wake wa kutumia kompyuta

DAR ES SALAAM: NI mfano wa kujitoa ili kuwa kioo kwa wale wote waliokata tamaa ya kujaribu, kisa tu wanaishi na ulemavu au watu wenye mahitaji maalum.

Raphael Mwambalaswa, msomi asiye na uwezo wa kuona. Kwa sasa ni Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) inayolenga kuhakikisha kila mtoto mwenye changamoto ya ulemavu wa uoni anapata mafunzo ya vitendo ‘functional skills’, jambo lililomsukuma kujiunga na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika fani ya ufundi aluminiam ‘aluminium works’ inayohusisha utengenezaji wa vifaa vya aluminiam.

SOMA: Wanafunzi 500 kupewa nafasi vyuo vya wenye ulemavu

“Msingi mkubwa wa ualimu vyuoni ni tafiti, hilo limenisukuma kuja VETA. Nimebaini elimu ya nadharia pekee haitoshi kuwainua watu wanaoishi na ulemavu,” amesema Mwambalaswa akiwa katika banda la VETA ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere kushiriki Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba 2024).

Kushoto ni
Raphael Mwambalaswa, msomi mwenye ulemavu wa macho sanjari na Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Ismaily Kawambwa

Mwambalaswa anasema si vyema kuwa mchoyo wa fadhila kwa kutowashukuru VETA kwa nafasi waliyompatia kujifunza sambamba na wanafunzi wengine wenye mahitaji maalum ikiwa ni Mradi wa Mfuko wa Waziri Mkuu.

Lakini, kilio chake kikubwa kinabaki kwa wenye mahitaji maalum waliojifungia majumbani na kushindwa kuzifikia fursa zilizopo ikiwemo fursa ya elimu stadi.

“Watu wenye mahitaji maalum wanahitaji kujitegemea,” amesisitiza Mwambalaswa.

Anasema, walimu wake hapo VETA wanafanya juhudi za makusudi kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wanapata elimu kwa wepesi ingawa ukweli ni kuwa vifaa vilivyopo toka kiwandani vingi havijaandaliwa kwaajili yao.
“Changamoto ya vifaa sio tu VETA, bali hata katika taasisi nyingine. Nafikiri kuna haja ya kulitazama hili,” amependekeza Mwambalaswa.

Amesema kwa sasa ana miezi mitatu tu chuoni hapo lakini kwa jitihada za walimu wake, amemudu kutambua vifaa vya ufundi kwa majina na hata matumizi.

Raphael Mwambalaswa akitengeneza katika shughuli ya ufundi aluminium

“Maumbo haya nimetengeneza mimi (ananionesha). Ninaweza kukata na kuunganisha aluminiam (ananionesha baadhi ya kazi alizofanya). Angalia hii, hapa ni wakati naanza anza na hii tazama,” anasema Mwambalaswa huku akiwa na furaha kwa namna anavyoendelea vizuri na mafunzo yake.

Salehe Omari, Mkufunzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Dar es Salaam katika Fani ya Ufundi Seremala (ndani yake kuna kozi ya muda mfupi ya aluminiam).

“Sisi tumempokea (Mwambalaswa) na ameshaanza kufanya mafunzo. Ni mwezi wa tatu sasa. Si yeye tu, tupo na wanafunzi wengine wenye mahitaji maalum,” amedokeza mkufunzi huyo akiwa katika banda la VETA.

Amesema, alipowasili chuoni hapo walimuandalia vipimo maalumu kupitia rula ya mkunjo ‘folding ruler’ na vifaa vingine ikiwemo ‘squere’.

Amesema tayari ameshaanza kutumia mashine nyinginezo baada ya kufaulu masomo ya vipimo.

“Kutokana na changamoto yake ya uoni, tulihakikisha anapotumia mashine, akiiwasha kuiacha mashinea mpaka mashine itakapazima au kuacha kutoa mlio,” amesema Omari wakati akielezea namna wanavyohakikisha usalama wa Mwambalaswa wawapo mafunzoni.

Amesema walimu wamekuwa wakiendelea kujifunza namna ya kumfundisha kupitia yeye mwenyewe (Mwambalaswa).

“Kinachofurahisha zaidi, anaweza kutumia kompyuta. Anatumia kifaa hiko kuchukua ‘notes’ waraka na kujifunzia,
“Ni rahisi kumfundisha kwakuwa tayari ana taaluma nyingine,” amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Abdallah Ngodu amesema wametengeneza miongozo mbalimbali ya elimu jumuishi ili kuwajumuisha pamoja wa hali zote ili kuwapatia elimu.

“Kwa sasa VETA tuna vyuo 80 vinavyotoa mafunzo na tumepanga kujenga vyuo vingine 65 kufikia mwakani tutakuwa na jumla ya vyuo 145 ili walau kila wilaya nchini iwe na chuo,

“Katika chuo chetu cha Dar es Salaam kilichopo eneo la Chang’ombe, tuna watu wenye mahitaji maalum ikiwemo wenye ulemavu mchanganyiko, miongoni mwao tumekuja nao katika maonesho haya,” amesema Ngodu.

Amesema wamekuwa wakishirikiana na wanafunzi wote kwa ukaribu na hata Mwambalaswa ni miongoni mwa wanafunzi wanaopata elimu katika misingi bora.

Akizungumzia kuhusu muitikio wa jamii kuleta watu wenye mahitaji maalimu, Ngodu amesema muitikio ni mzuri na bado wanaendelea kuhamasisha.

“Muitikio ni mdogo lakini walau wanakuja. Tulilenga kupata wanafunzi 1000 lakini wamepungua hadi kufikia 400,” amesema mkurugenzi huyo.

Tukirejea kwa, Mwambalaswa amesema muitikio wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ni mdogo hata hivyo ameiomba serikali kuboresha miundombinu ili kuwa rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Habari Zifananazo

Back to top button