Fundi mashine za EFD, wenzake 3 kortini kuisababishia TRA hasara

FUNDI wa mashine za kielektroniki za EFD, Awadhi Mhavile (39) na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashitaka saba yakiwamo ya kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh milioni 954.5.

Washitakiwa wengine ni Ally Msesya maarufu kama Ally Yanga (37) fundi na Mkazi wa Pugu na Salma  Ndauka (38), mkazi wa Sinza na msimamizi wa gereji.

Wote kwa pamoja wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka saba mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Medalakini akisaidiana na Wakili wa Serikali, Auni Chilamula, wamedai kuwa kati ya Mei 17 na Julai mwaka huu, maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja walitumia isivyo halali mashine za kielektroniki za EFD zilizofungiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  na kutoa risiti zilizowanufaisha walipa kodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh 954,596,372  na kumpotosha Kamishna wa mamlaka hiyo.

Pia inadaiwa katika tarehe na mwezi huo, washitakiwa wote kwa pamoja walitumia mashine  zilizofungiwa kumdanganya Kamishna na kutoa risiti zisizo sahihi na kuwanufaisha walipa kodi wengine kudai Sh 954,596,372.

Medalakini amedai mashitaka ya tatu yanamkabili Mhavile ambapo inadaiwa Julai 8 mwaka huu, mshitakiwa huyo alikutwa na mashine za kielektroniki 22 zidhaniwazo kuwa za wizi  au kuchukuliwa kinyume na sheria.

Amedai Julai 19, mwaka huu maeneo ya Sinza A, Wilaya ya Kinondoni, Ndauka alikutwa na mashine 10 za EFD zidhaniwazo kuwa za wizi au kuchukuliwa kwa njia ya isivyohalali.

Katika mashitaka ya tano yanamkabili Mhavile, inadaiwa Julai 8 mwaka huu maeneo ya Lumumba mkoani Dar es Salaam, alikutwa na mashine 10 za EFD na kutoa risiti za kielektroniki kinyume na sheria.

Medalakini ameendelea kudai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja kati ya Mei 13 na Julai mwaka huu mkoani Dar es Salaam, washitakiwa Mhavile, Ndauka na Msesya waliisababishia serikali (TRA) hasara ya Sh milioni 954.5.

Katika mashitaka ya saba ya utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Mei 13 na Julai mwaka huu mkoani Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa kutumia mashine hiyo walitoa risiti zisizohalali zilizotumiwa na walipakodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh milioni 954.5 kwa TRA wakati wakijua kwamba fedha hizo ni zao la kuisababishia serikali hasara.

Hakimu Kiswaga amewataka washitakiwa hao kutojibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na kwamba haijapewa kibali na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Pia amesema kwa mujibu wa sheria  kifungu cha 148(5)(a) kinataja makosa ambayo hayapaswi kupewa dhamana ikiwemo utakatishaji fedha.

Amesema washitakiwa wataendelea kukaa rumande hadi Agosti 21 mwaka huu kesi yao itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Habari Zifananazo

Back to top button