Gamondi:Inawezekana kuishangaza Mamelodi

DAR ES SALAAM: KOCHA wa Yanga Miguel Gamondi amesema timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyopangwa kucheza na Yanga hatua ya robo Fainali na timu ya Aly Ahly ya Misri iliyopangwa kucheza na Simba hatua hiyo zinapaswa kucheza fainali kwa kuwa ni timu kubwa na zenye uzoefu wa mashindano hayo na pia zina uwekezaji mkubwa wa kifedha.

Amesema Mamelodi wanauchumi mkubwa akitolea mfano kwenye dirisha dogo Mamelodi wamenunua mchezaji kutoka Argentina kwa fedha nyingi wakati Yanga imewasajili Guede na Okra kwa gharama za kawaida tofauti na Mamelodi.

Akizungumzia kuhusu kushindana na Mamelodi, kocha huyo amesema kwa kuwa watakuwa wachezaji 11 kwa 11 watapambana kusaka ushindi bila kujali uwezo wao wa kifedha ama uzoefu wao katika mashindano makubwa ingawa amesema changamoto kubwa aliyoioana kwa wachezaji wengi wa Tanzania wamekosa uzoefu wa mashindano makubwa.

“Uzoefu ndiyo ulikuwa kitu pekee kilichotutofautisha na Aly Ahly tulifanya makosa nyumbani na tukafanya makosa kwao Misri lakini Aly Ahly hawakufanya makosa hii inaonyesha ukikosa uzoefu wa mechi za kimataifa uwezekano wa kutengeneza makosa ni mkubwa tofauti na timu zenye uzoefu wa mechi za kimataifa,” amesema Gamondi.

Gamondi ambaye aliwahi kufanyakazi na Mamelodi Sundowns mesema mechi yao na Mamelodi inaweza kuwashangaza wengi na itakuwa furaha sana wakifuzu nusu fainali tena kwa kuwatoa Mamelodi lakini wakishindwa itakuwa historia nzuri kwao kucheza na Mamelodi na pia watakuwa wamepata uzoefu wa kucheza na timu kubwa kama Mamelodi.

“Mamelodi wanacheza kama sisi na kwa Yanga ni nafasi nzuri kucheza na timu kubwa kwani kama tunataka kuwa wakubwa kwa Afrika lazima tucheze na timu kubwa kama Mamelodi,” amesema Gamondi.

Ameongeza soka la Tanzania limenyanyuka sana baada ya timu mbili Simba na Yanga kuingia hatua ya robo fainali.

Pia Gamondi amesema hafikilii makubwa sana katika mashindano hayo kwa kuwa anapenda kwenda hatua kwa hatua huku akidai kwamba mpango wao ulikuwa ni kuendelea kushinda kombe la ligi, FA na kuingia makundi lakini walivyofanikiwa zaidi ikawalazimu kupambana na timu kubwa ikiwemo Aly Ahly na CR Belouzdad na wakashinda licha ya bajeti zao kuwa kubwa.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button