Gavana Taliban auawa shambulizi la kujitoa mhanga

Gavana wa Taliban wa jimbo la Balkh kaskazini mwa Afghanistan, Mohammad Dawood Muzammil ameuawa katika shambulio la kujitoa mhanga linalodaiwa na kundi la Islamic State (IS). Shirika la Habari la Aljazeera limeeleza.

Kiongozi huyo ameuawa katika ofisi yake iliyopo mji Mkuu wa Mkoa, wa Mazar-e Sharif jana. Muzammil ndiye afisa mkuu wa Taliban kuuawa tangu wanamgambo hao warejee mamlakani mwaka 2021.

Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid alisema kwenye Twitter kwamba gavana huyo “aliuawa shahidi katika mlipuko wa maadui wa Uislamu”.

Muzammil alikuwa ameongoza vita dhidi ya IS katika wadhifa wake wa awali kama gavana wa jimbo la mashariki la Nangarhar. Alihamishiwa Balkh Oktoba iliyopita.

Msemaji wa polisi wa Balkh Mohammed Asif Waziri alisema mlipuko huo ulitokea Alhamisi asubuhi kwenye ghorofa ya pili ya ofisi ya gavana.

“Kulikuwa na kishindo. Nilianguka chini,” Khairuddin, ambaye alijeruhiwa katika mlipuko huo, aliliambia shirika la habari la AFP. Alisema ameona rafiki yake akipoteza mkono katika mlipuko huo.

Habari Zifananazo

Back to top button