TIMU ya Geita Gold Fc ya mjini Geita imeweka wazi kuwa kusitishwa kwa matangazo mubashara ya runinga kwa michezo ya ligi ya championship huenda ikarudisha nyuma ubora na ushindani wa ligi hiyo.
Ofisa Habari wa Geita Gold Fc, Samwel Didda amesema hayo katika mahojiano maalum na HabariLeo ambapo alitoa kauli hiyo baada ya runinga ya TV3 kusitisha matangazo mubashara ya championship.
Didda amesema michezo inapokuwa mubashara inaongeza ufanisi wa waamuzi wa michezo na kuchagiza molari ya wachezaji kwani wanakuwa wanaonekana kwenye hazira kubwa ya wadau wa soka.
“Michezo inapokuwa hazarani ama hazira inaona kunakuwa na ufanisi mkubwa, sasa kama hazira haioni, huenda kuna vitu vingi vinafanyika vingine vinaweza vikawa vya haki vingine visiwe vya haki”, amesema.
Amesema ligi ya championship kwa sasa imefikia kwenye ushindani mkubwa kama ilivyo kwa ligi kuu ya Tanzania bara kwani igi zote kwa sasa zinabadilishana wachezaji kupitia usajili bila mashaka yeyote.
“Hii ligi imekua sana, ushindani umeongezeka, wachezaji waliopo Championship wana karibiana kiwango sawa na wale wanaocheza ligi kuu, wanatofautiana vitu vidogo tu.
“Ndiyo maana sasa hivi mchezaji wa ligi kuu kwenda kucheza championship siyo inshu tena, anakuja tu kucheza na ni safari ambayo anaweza kuitumia kurudi kwenye ubora wake”, amesema Didda.
Ameongeza kuwa, michezo ya Championship inapokuwa mubashara kupitia ruinga inatoa fursa kubwa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao na kuweza kuonekana ili kufikia ndoto zao kwenye soka.
Amesema pia championship kuonekana mubashara kupitia runinga inaongeza thamani ya ligi kwa kuhamasisha wawekezaji na wadhamini ambao dhamira yao kuu ni kutangaza bidhaa zao kupitia soka.
“Tuna watu wameweka fedha yao kupitia udhamini, kwa hiyo wanatamani kuona pia wanaonekana kupitia runinga, ili mashabiki waone bidhaa ambazo zipo ndani ya timu.
“Kama haifanyiki hivo maana yake mnakuwa mnawanyima haki ya kuonekana watu wanaowapa pesa, pia inapunguza ufanisi ndani ya ligi kwa sababu kuna vitu vingi vinakuwa vinafanyika nyuma ya pazia”, amesisitiza.
Didda ameziomba mamlaka zinazosimamia soka nchini kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha matangazo mubashara ya runinga kwa ligi ya Championship yaweze kurejea na kama ilivyokuwa hapo awali.