Geita Gold yaitaka Ligi Kuu Tanzania Bara

TIMU ya Geita Gold ya mjini Geita imejipambanua kuwa ipo tayari kuanza mapambano ya kurudi Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na uwekezaji mkubwa ulioufanya kwenye kikosi chake.

Kocha wa Geita Gold Amani Josiah amesema hayo leo wakati akizungumza kuelekea mchezo wa timu hiyo wa ligi ya Championship dhidi ya TMA ya Arusha utakaochezwa Septemba 21 Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

Amesema malengo makuu ya timu ni kurejea Ligi Kuu na kwamba maandalizi makubwa yamefanyika huku kazi kubwa iliyosalia ni wachezaji kutekeleza wajibu wao ndani ya uwanja.

SOMA: Geita Gold haitanii usajili mpya

“Mimi kama mwalimu nimejitahidi timu iwe na wachezaji ambao ni wazuri, wachezaji wakubwa ambao wanaweza kuchukua mawazo yangu na wakayaweka uwanjani.

“Dhima ya mechi hii (dhidi ya TMA) sisi tunahitaji kushinda, hatuna sababu nyingine kwamba hatuwezi kushinda mechi hii ya nyumbani kwa maandalizi ambayo tumefanya, kwa ubora tulionao,” amesema Josiah.

Amesema, kabla ya kuanza kwa Ligi ya Championship Geita Gold imecheza michezo sita ya kirafiki ikishinda michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja matokeo yanayodhihirisha ubora wa kikosi hicho.

Nahodha wa Geita Gold, Frank Magingi amesema wanaheshimu kila mpinzani watakayekutana naye ikiwemo TMA ambapo wamejipanga kuhakikisha wanaianza vizuri safari ya kurejea Ligi Kuu.

Kocha Msaidizi wa TMA, Augustine Thomas amesema wanaiheshimu Geita Gold kama timu iliyotoka ligi kuu lakini kupitia mbinu za kiufundi hawapo tayari kuanza ligi kwa kupoteza mchezo wa kwanza kwa kuwa hawataki kurudia makosa ya msimu uliopita.

Amesema huu ni msimu wa pili katika Ligi ya Championship baada ya kumaliza nafasi ya tano katika msimu wa kwanza ambapo wamepata uzoefu wa kutosha kushindana.

Nahodha Msaidizi wa TMA, Gabriel Lusingo amekiri ushindani kwenye Championship umeongezeka lakini hilo haliwapi uoga wa kuikabili Geita Gold kwenye mchezo wao wa kwanza.

Habari Zifananazo

Back to top button