Geita kuongeza weledi usimamizi miradi ya maji

MKUU wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amesema wilaya hiyo imejipanga kupunguza utitiri wa Vyombo vya Watumiaji Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) ili kuongeza weledi katika usimamizi wa miradi ya maji.

Magembe amesema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa vyombo vya watumiaji maji wilayani Geita ulioandaliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijjini (RUWASA).

Amesema hatua hiyo inakuja kufuatia kubainika uwepo wa jumuiya nyingi za watumiaji maji ambazo zimeshindwa kujiendesha badala yake zinazimama kwa kutegemea pesa mbichi za mauzo ya maji.

Amesema mpaka sasa tathimini inaonyesha wilaya ina jumla ya CBWSOs 19 lakini zenye uwezo wa kujiendesha ni saba pekee hivo wameandaa mpango wa kuziunganisha kuondoa utitiri wa CBWSOs.

“Lengo la Ruwasa ni kuwa na vyombo vichache yaani walau chombo kimoja kwa kila tarafa vitakavyokuwa na watalaamu wenye sifa na ikibidi vitendea kazi kama magari na pikipiki.”

Amesema kiini cha jumuiya nyingi za maji kushindwa kujiendesha ni makusanyo hafifu ya fedha za mauzo ya maji tatizo linalotokana na uelewa mdogo wa masuala ya fedha na matumizi yake kwa watendaji.

Ameeleza CBWSOs kutatua changamoto za kiuendeshaji wa shughuli za maji ili miradi iweze kuwa endelevu kwani serikali inagharimikia fedha nyingi katika ujenzi wa miradi hiyo ya maji.

“Vipo baadhi ya vyombo ambavyo havina uwezo wa kugharamia matengenezo ya miundombinu katika maeneo yao na pia havina uwezo wa kuajiri watalaamu wenye siafa za kusimamia miradi husika.”

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Geita, Mhandisi Sande Batakanwa amesema mpaka sasa hali ya upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijijni ni asilimia 36 na inaendelea na mradi wa dharura wa uchimbaji visima virefu.

Sande amesema mradi tayari umeshaanza kutekelezwa kwenye baadhi ya maeneo na hatua zinaendelea kuvifikia vijiji vyote vyenye uhitaji wa huduma ya maji.

Ofisa Ukaguzi wa Ndani halmashauri ya wilaya ya Geita, Chacha Masero ameiomba Ruwasa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kudhibiti upotevu wa mapato ya maji.

Habari Zifananazo

Back to top button