SERIKALI imeahidi kuwasaka, kuwakamata na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria watu wote wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya maofisa uhamiaji wawili katika kijiji Mtakuja, Kata ya Lulembela wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigell,a wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali katika ibada ya kuaga miili ya marehemu iliyofanyika wilayani Bukombe.
Askari waliouawa ni Mkaguzi wa Jeshi la Uhamiaji, Salum Msongela (32) na Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji, Gilbert Edward (42) na mwananchi, mmoja ambapo waliuawa usiku wa Oktoba 26, 2022 wakati wakitekeleza majumu ya kikazi.
Amesema serikali inatambua askari hao walikuwa wanafuatilia wahamiaji haramu waliokuwa wamehifadhiwa na mmoja wa wananchi kijijini humo, hivyo kilichofanywa na wananchi ni kupingana na majukumu ya serikali.
“Nitumie nafasi hii kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha wale wote waliohusika awe ni kiongozi, awe mwananchi wa kawaida wote wanakamatwa.
“Kwetu sisi kama serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, tunaona hii ni changamoto, lakini changamoto ambayo inatupa nguvu ya kuona vita hii ni kubwa, kwa hiyo lazima tuweke jitihada kubwa, na nguvu zaidi katika kupambana na uharifu,” amesema.
Shigella amewataka wananchi na viongozi wa mitaa, vijiji na kata kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha uchunguzi, huku akiwaonya wote wanaohifadhi wahamiaji haramu kuacha kwani watashughulikiwa.
Naye Kamishina wa Uhamiaji na Udhibiti wa Mipaka nchini, Samwel Mahirane, akizungumuza kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, amesema tukio hilo halitowarudisha nyuma badala yake wataongeza nguvu zaidi kubaini wahamiaji haramu.