Geita yatakiwa kuja na mradi wa Kaboni kuokoa mazingira
GEITA: MKOA wa Geita umetakiwa kuanzisha mradi wa kaboni ili kujipatia kipato na kukabiliana na kasi ya uharibifu wa mazingira inayotokana na shughuli za ukataji wa miti hovyo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa maelekezo hayo akiwa wilayani Chato katika maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani.
Maadhimisho hayo kwa mikoa ya kanda ya ziwa yamefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) ambapo yaliambatana na zoezi la usafi wa mazingira na upandaji miti hospitalini hapo.
Mhandisi Luhemeja amesema mbali na upandaji miti unaofanyika kwenye maeneo tofauti bado hakuna mpango madhubuti wa kusimamia miti hiyo na kuigeuza fursa kiuchumi kupitia mradi wa kaboni.
Amesema Geita ni miongoni mwa mikoa iliyoathirika kwa kiwango kikubwa na ukataji wa miti na kupelekea mabadiliko ya tabia ya nchi na hata kuhatarisha uhai wa misitu na umbijani.
Mhandisi Luhemeja amesema yupo tayari kwenda Geita kutoa somo la biashara ya kaboni ili kusaidia kurejesha misitu iliyopotea kwani athari ni kubwa na hatua zisipochukuliwa ni hatari kwa kizazi kijacho.
“Miti sasa hivi ni biashara inayogeuka, tunahamasisha biashara ya Kaboni (carbon)kila mti mmoja unaoupanda unazalisha Oksijeni na mti mmoja unaoupanda unakula Karboni.”
Ametolea mfano Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Kigoma ambayo Juni 05, 2024 itapatiwa cheki ya Sh bilioni 14 kutokana na mradi wa kaboni na hivo linaweza kuwa somo kwa wengine.
“Niwaombe muangalie namna ya kutumia hii fursa, ambapo hii miti sasa tunayoipanda naomba tuongeze nguvu kwa mwananchi mmoja mmoja, kikundi cha watu na jamii kwa ujumla.”
Aidha amelitaka mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Geita, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara na Simiyu kusimamia zoezi la kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka kudhibiti jangwa.
“Ofisi ya Makamu wa Rais tumeanza mchakato wa kutoa zawadi kwa halmashauri iliyofanya vizuri, kwa mkoa uliofanya vizuri, na hili zoeizi linaanza mwakani na mkoa uliofanya vibaya tutausema.”
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela amekiri kukithiri kwa upotevu wa misitu mkoani Geita huku akitaja shughuli za uchimbaji wa madini kuwa kiini cha tatizo kutokana na matumizi makubwa ya miti.
Ameagiza kila halmashauri kusimamia urejeshaji wa uoto wa asili kwenye maeneo baada ya shughuli za uchimbaji madini na kuahidi kuandaa kikao maalum kuona namna gani ya kuja na biashara ya kaboni.