GEN-Z watatu Kenya waachiliwa

KENYA : RAIA watatu waliotekwa wakati wa maandamano ya vijana wa Gen-Z nchini Kenya wameachiliwa huru.
Mashirika ya haki za binadamu nchini humo yamevishutumu vikosi vya usalama kwa kutotoa taarifa ya eneo walikokuwa wameshikiliwa.

Watu hao, waliofahamika kama Bob Njagi, Aslam Longton na kaka yake Jamil Longton, wanadaiwa kutekwa mnamo Agosti 19 na wanaume waliojitambulisha kuwa maafisa wa polisi katika eneo la Kitengela, karibu kilomita 30 kusini mwa mji mkuu, Nairobi.

Hivi karibuni, tukio hilo lilipamba moto baada ya mahakama mjini Nairobi kumtia hatiani naibu mkuu wa jeshi la polisi, Gilbert Masengeli, kwa kosa la kudharau mahakama, kutokana na kushindwa kutokea mahakamani ili kujibu maswali juu ya kutoweka kwa watu hao watatu.

Advertisement

SOMA  : Polisi Kenya wapiga marufuku maandamano Nairobi

Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi (IPOA) imesema inachunguza malalamiko kadhaa ya ukamataji wa kinyume cha sheria na utekaji kufuatia maandamano makubwa ya kuipinga serikali yaliozuka nchini Kenya mwezi Juni.