Polisi Kenya wapiga marufuku maandamano Nairobi

Kaimu Mkuu wa Polisi Kenya, Douglas Kanja Kirocho.

JESHI la Polisi Kenya limepiga marufuku maandamano katika eneo la katikati ya mkuu wa nchi hiyo, Nairobi hadi itakapotangazwa tena kufuatia wiki kadhaa za maandamano dhidi ya serikali ambayo limesema yamevamiwa na magenge ya wahalifu.

Kabla ya marufuku hiyo, mabango kadhaa yamesambwzwa mtandaoni yakihimiza waandamanaji kukusanyika katika uwanja wa Uhuru uliopo jijini humo kabla ya kuelekea Ikulu leo.

Biashara jijini Nairobi zimebaki zimefungwa kwa hofu ya kurejea kwa uporaji uliofanyika wakati wa maandamano wiki iliyopita, ambapo waandamanaji walivamia Bunge na baadhi yao kuuawa na polisi.

Advertisement

Watu wapatao 50 wameuawa katika maandamano yanayoongozwa na vijana wanaojulikana kama ‘Gen Z‘ kupinga ongezeko la kodi lililopendekezwa, ambayo yalizuka kote nchini humo mmoja uliopita na yameendelea hata baada ya Rais William Ruto kuondoa muswada wa sheria ya kodi na kuvunja baraza lake la mawaziri.

SOMA: Gen Z waingia tena mitaani Kenya

Waandamanaji wanamtaka Rais Ruto ajiuzulu na kufanyika mabadiliko ya kimsingi ili kupambana na rushwa na kushughulikia uongozi mbovu.

“Tuna taarifa za kuaminika kuwa magenge ya wahalifu yamepanga kutumia maandamano yanayoendelea kutekeleza mashambulizi yao ikiwa ni pamoja na uporaji,” amesema Kaimu Mkuu wa Polisi Douglas Kanja Kirocho.

Maandamano hayo, ambayo yameandaliwa mtandaoni bila msaada wa wazi wa viongozi wa kisiasa wa upinzani, yamezua mgogoro mkubwa zaidi katika miaka miwili ya Rais Ruto madarakani.

Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imevionya vyombo vya habari dhidi ya kuchochea vurugu katika taarifa zao.

“Baadhi ya vituo vimepoteza weledi na usawa katika kuripoti uhalifu na hali za mizozo,” amesema mkuu wa CA David Mugonyi katika barua ya Julai 17.

Yalianza kwa amani lakini baadaye yakawa na vurugu. Waandamanaji kadhaa walivamia majengo ya bunge kwa muda mfupi Juni 25 hali ilisababisha polisi kufyatua risasi.

Ofisi ya Rais Ruto ilipanga mazungumzo ya sekta kadhaa wiki hii ili kushughulikia malalamiko ya waandamanaji, lakini hakuna dalili kuwa yameanza.

Watu wengi wanaoongoza maandamano hayo wamekataa mwaliko huo, badala yake wanataka hatua za haraka juu ya masuala kama rushwa.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya ilisema tangu tarehe 18 Juni, watu 50 wamefariki katika maandamano, huku wengine 59 wakitekwa na kutoweka.