Great Ruaha Marathon kuongeza pato Iringa

KITENDO cha watu zaidi ya 350 kujitokeza kushiriki mbio za mwendo wa pole na haraka (Great Ruaha Marathon) zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Julai 8, mwaka huu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha zimetajwa kuwa sababu ya kuongeza pato la Mkoa wa Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amewapongeza waandaji wa mbio hizo, Shirika la Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) akisema zitasaidia kuchochea pia utalii, uhifadhi na uwekezaji na katika mkoa wake.

“Milango ya kushiriki mbio hizi haijafungwa, naomba watu wajitokeze zaidi. Michezo ni uhai, uchumi na ukuza urafiki na undugu,” amesema leo mjini Iringa wakati akikabidhiwa vifaa vitakavyomuwezesha kushiriki mbio hizo.

Advertisement

Mbali na kukuza utalii wa kusini, Dendego amesema mbio hizo zinazotarajiwa kuzinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengelwa zitatumika kuhamasisha uhifadhi wa maliasili vikiwemo vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji yake kuelekea Mto Ruaha Mkuu.

Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meing’ataki amesema mto Ruaha Mkuu ni chanzo kikuu cha maji kinachotegemewa kwa ajili ya uhai wa wanyama wa hifadhi hiyo.

Amesema mtiririko wa maji katika mto huo umekuwa ukiathiriwa na shughuli za kibinadamu zinazofanywa kwenye vyanzo vyake na wakati fulani kuleta madhara makubwa vikiwemo vifo kwa baadhi ya wanyama.

“Ni matarajio yetu mbio hizi kwa upande mwingine zitatumika kuihamasisha jamii kuvilinda vyanzo hivyo kwa uhai wa wanyama wa hifadhi na uchumi wa Taifa kwa ujumla wake na kutangaza vivutio vilivyopo katika hifadhi yetu,” amesema.

Amesema hifadhi yao imejipanga vizuri kwa malazi, chakula na ulinzi wakati wote wageni watakapowasili na muda wote watakaokuwepo hifadhini kushiriki mbio hizo.

Mratibu wa mbio hizo kutoka shirika la SYDP linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya afya, stadi za maisha, ujasiriamali kwa vijana na hifadhi na utunzaji wa mazingira Hamimu Kilahama amesema Mbio hizo zitakazoanzia daraja la Mto Ruaha (Ibuguziwa), zitafanyika kwa umbali wa kilometa 5, 10, 21 hadi 42. 

“Maandalizi kuelekea mbio hizi yanakwenda vizuri na ni matarajio yetu zitafanikiwa sana na kuamsha hali ya watanzania kutembelea vivutio vyao lakini pia kuwa sehemu ya uhifadhi ili viendelee kuwepo kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo,” alisema.

Mbali na hoteli maarufu ya Mabata Makali Lodge and Campsite kujitokeza kudhamini mbio hizo, Kilahama alisema Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) nao wameweka mkono wao kuhakikisha zinapata mafanikio yanayotarajiwa.

Ofisa wa TTB Kanda ya Iringa, Hoza Mbura alisema utalii wa michezo ni moja ya mbinu ambayo bodi yao inatumia kutangaza utalii ndani na nje ya nchi.

“Katika kufikia lengo hili TTB tunashirikiana wadau mbalimbali kama hawa kuhakikisha vivutio vyetu vinatangazwa na vinatembelewa. Niwapongeze waandaji kwa kuja na mbio hizi,” alisema.

1 comments

Comments are closed.

/* */