‘Hakikisheni Tanzania inaongoza kwenye Tehama’

‘Hakikisheni Tanzania inaongoza kwenye Tehama’

SERIKALI imeitaka Tume ya Tehama nchini, kuhakikisha Tanzania inaongoza kwenye Tehama katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ili kuwa  mfano  kwenye sekta hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Jim Yonazi, alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Tume ya Tehama, kwa ajili ya kuwakutanisha wabunifu mbalimbali nchini.

Amesema ni muhimu kwa wabunifu wote kusaidiwa, ili kufanya vizuri na kuwe na muunganiko na kuunganishwa na taasisi za elimu, ili kuendelea kupata elimu itakayowasaidia kuwatoa pale walipo na kusonga mbele zaidi, ili kukuza vipaji  nchini.

Advertisement

Dk Yonazi amesema, serikali  imejipanga kufanya  kongamano la Tehama,  Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kuwezesha wafanyabiashara kufahamu utaalam walionao Watanzania kwenye eneo la tehama.

Amesema vipo vikwazo vya kisera na kikodi  wanavyokumbana navyo wabunifu katika Tehama, ambavyo kwa namna moja hadi nyingine  haviruhusu  ubunifu kufanya kazi.

Dk Yonazi amesema Tanzania inatamani kuwa na mfumo wa ubunifu na ambao lazima utashirikisha wadau husika, hasa kuelekea  kwenye uchumi wa kidigitali.

“Kwa nchi yetu kuna kuna changamoto ya ajira, hivyo kupitia ubunifu katika Tehama tatizo hilo linaweza kupatiwa ufumbuzi, kwa kuwa wapo wabunifu walioweza kutoa ajira kwa wengine,” amesema Dk Yonazi na kuwataka wabunifu kufahamu kuwa  hakuna mafanikio bila kuwa na nia.

Amesema Wizara ya habari inaendelea kufanyia kazi namna ya kuwatambua wabunifu katia Tehama, lakini pia inaendelea kutengeneza vituo vya ubunifu nchini ifikapo mwaka 2025 katika mikoa mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Tehama , Dk Nkundwe Mwasaga, amesema tume hiyo imekutana na wabunifu, ili kujua  changamoto wanazokumbana nazo na  namna ya kukabiliana nazo, ili  kukuza sekta hiyo na iweze kukuza uchumi na kuajiri wengine.

Amesema nia ya tume ni kuwa na vituo vya Tehama kwa kila wilaya nchini, kwa kuwa ni eneo ambalo linashindana kwenye kukuza uchumi wa Tanzania.