WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ratiba ya kufunguliwa shule kesho ipo vilevile kwa mujibu wa waraka wa elimu Na 2 wa mwaka 2022 kuhusu mihula ya masomo.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa bodi ya Shule ya Sekondari ya Ole iliyopo katika Mkoa wa Kusini Pemba wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mjini Pemba.
Kauli hiyo ya Profesa Mkenda inatokana na taarifa za uzushi kuhusu tarehe ya kufunguliwa shule zilizotolewa na baadhi ya watu.
Taarifa hizo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii zilisema kuwa shule zitafunguliwa Septemba 21, mwaka huu jambo ambalo waziri alisema si kweli na kwamba hakuna mwongozo wala maelekezo hayo.
Alieleza kuwa ratiba ya kufunguliwa shule ipo vilevile kwa mujibu wa waraka wa elimu Na 2 wa mwaka 2022 kuhusu mihula ya masomo uliotolewa na Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Lyabwene Mtahabwa.
“Naomba mpuuze jambo hili kwanza aliyesambaza anatumia nembo ya kampuni moja ambayo kampuni hiyo haijui na haihusiki na tangazo hilo, kwa hiyo hakuna maelekezo yoyote zaidi ya yale yaliyotolewa na kamishna wa elimu,” alisema.
Kuhusu mageuzi ya elimu, Profesa Mkenda alisema kuwa serikali inafanya mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 pamoja na mapitio ya mitaala ili kuboresha sekta ya elimu.
Alisema kuwa Tanzania, Zanzibar na Tanzania Bara zinafanya kwa pamoja mapitio hayo kwa karibu ili kupata mawazo ya wadau wa elimu na wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inaboresha elimu hususani kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi wanakuwa na elimu ufundi na elimu ujuzi.