‘Hakuna ongezeko tozo za maegesho’

ARUSHA: Wananchi wa Jiji la Arusha wametakiwa kuwa na imani kuwa hakuna ongezeko la viwango vya tozo za maegesho ya magari litakalofanyika, huku Kampuni ya Rick Plan Co. Ltd ikiahidi kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa huduma hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Haroub Mlapakolo, amesema lengo la kampuni si kuongeza mzigo kwa wananchi, bali kuhakikisha maeneo yote ya jiji yanafikiwa na mfumo wa ukusanyaji wa mapato unakuwa wenye ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mlapakolo alisema viwango vya tozo vitaendelea kubaki kama vilivyowekwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa mujibu wa sheria na kanuni.

“Hatutabadilisha kiwango cha ukusanyaji. Tozo zitabaki kama zilivyowekwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha. Kilichobadilika ni mpango wa utekelezaji ili kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa,” alisema.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora huku halmashauri ikiendelea kupata mapato yatakayosaidia katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo ya jiji.

Mlapakolo alisema kampuni imeanza mikakati ya kufikia maeneo ambayo awali hayakuwa yakihudumiwa ipasavyo katika ukusanyaji wa mapato, pamoja na kuweka mkazo katika ukusanyaji wa madeni ya nyuma kutoka kwa wadaiwa.

Kwa upande wa wafanyakazi, alisema kampuni itaendelea kutumia uzoefu wa baadhi ya wakusanyaji waliokuwepo awali huku ikiongeza nguvu kazi kulingana na mahitaji ya maeneo mapya.

Alisema pia mfumo wa usimamizi umeboreshwa kwa kuligawa Jiji la Arusha katika kanda mbalimbali, ambapo kila eneo litakuwa na msimamizi atakayefuatilia utendaji wa wakusanyaji ili kuongeza uwajibikaji.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma za maegesho zinaendeshwa kwa ufanisi zaidi na kuchangia ongezeko la mapato ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa manufaa ya wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button