Hali ni Shwari Ziwa Victoria
MWANZA: IMEELEZWA kuwa hali ya ulinzi na usalama ndani ya ziwa Victoria imeendelea kuimarika tofauti na miaka ya nyuma kutokana na tathimini zilizofanyika kupitia vikao vitano vilivyohusisha Maofisa wa Jeshi la Polisi, maafisa uvuvi pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na ulinzi wa rasilimali ndani ya ziwa hilo.
Taarifa hiyo imetolewa Oktoba18,2023, na Mkuu wa Usimamizi wa Vikosi Maalum vya Polisi kutoka Kamisheni ya Opereseheni na Mafunzo, Makao Makuu ya Polisi Dodoma (DCP), Ferdinand Mtui katika kikao maalum kilichowakutanisha Makamanda wa Jeshi la Polisi kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa na wadau wa uvuvi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni za Jeshi la Polisi Nchini, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mihayo Msikhela amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2019-2020 kuliibuka uhalifu ndani ya ziwa Victoria ikiwemo mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, uporaji wa nyavu, samaki na boti za Injini.
SACP Mihayo aliongeza kuwa vitendo hivyo vilipelekea majeruhi na vifo kwa baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara ziwani lakini kwa sasa matukio hayo yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Aidha katika hatua nyingine SACP Mihayo aliongeza kuwa sheria za Nchi zimeweka bayana iwapo mtu akiingia Nchini kinyume cha utaratibu ikiwemo kukosa kibali cha kusafiria atakamatwa na kufikishwa mahakamani huku akiwasisitiza wavuvi wa Tanzania wasivuke mipaka ya ziwa Victoria kwenda katika maeneo ya Nchi jirani za Kenya na Uganda.
Awali akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi ameeleza kuwa sekta ya uvuvi inachangia kwa asilimia saba ya pato la Mkoa.
Amesema kuwa Mkoa wa Mwanza umedhamiria kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano katika sekta ya uvuvi ya kuifanya Mwanza kuwa na uchumi wa bluu kwa kuanzisha miradi mbalimbali kupitia ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.