KILIMANJARO:Halmashauri ya wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, imekusanya Sh bilioni 3.8 sawa na asilimia 109 ya makusanyo ya ndani ikilinganishwa na lengo la Sh bilioni 3.5 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Moris Makoi amesema hayo, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi ya halmashauri kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 30 mwaka huu.
Makoi amewashukuru madiwani na wakuu wa idara kwa ushirikiano na juhudi walizofanya katika kukusanya mapato na kuzidi lengo walilojiwekea.
“halmashauri ilikusanya na kupokea mapato ya Sh bilioni 72 sawa na asilimia 98.6 ya lengo pia tumefikia asilimia 109 ya makusanyo kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani sawa na Sh bilioni 3.8 ikilinganishwa na lengo la Sh bilioni 3.5 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh milioni 322.7” amesema .
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa, Shaban Mchomvu amewapongeza kwa kumaliza mwaka wa fedha kwa kukusanya mapato ya kutosha na kupata hati safi na kuwataka waongeze vyanzo vipya vya mapato ili wafanye vizuri zaidi.
Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Moshi, Ramadhani Mahanyu amesema katika utekelezaji wa miradi, wahakikishe wanapeleka fedha kulingana na uhitaji wa kata husika ili kuhamasisha wananchi wachangie kwenye miradi hiyo.