Halmashauri yaanza kufuatilia marejesho nyumba kwa nyumba

Mfanyabiashara asimulia alivyotapeliwa mil 130/-

HALMASHAURI ya Mji wa Geita imeanzisha ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo isiyo na riba kwa makundi maalumu, nyumba kwa nyumba ili kuwabaini wadaiwa sugu na kukamilisha marejesho ya deni la Sh bilioni 1.26.

Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Prisca Rupia alibainisha hayo juzi alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli ya utoaji na usimamizi wa mikopo ya vikundi maalumu.

Prisca alisema kwa kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi April, 2022 halmashauri ilikuwa inadai Sh bilioni 2.03 lakini hadi kufikia Desemba 15, 2022 halmashauri ilikusanya Sh milioni 763.6.

Advertisement

Alieleza ufuatiliaji wa deni unajumuisha watendaji wa mitaa, vijiji na kata kwa ushirikiano na jeshi la akiba na polisi ambapo wadaiwa sugu wanaobainika kukaidi kulipa deni wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Kuanzia Julai hadi Desemba tumetenga kiasi cha shilingi milioni 440 ambapo tunatoa shilingi milioni 387, sawa na asilimia 87.9 kwa vikundi 33 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” alisema.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu aliiomba ofisi ya maendeleo kuhakikisha inasimamia vikundi vinavyopokea mikopo ili malengo ya kutoa Sh milioni 906 kwa mwaka huu wa fedha yawe na tija.

“Tumeshauri idara hii iimarishe mfumo wa kufuatilia, kwa sababu tunaposhindwa kudai hawa, tunashindwa kuwapa wengine,” alisema

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi aliwaomba wanufaika wa mikopo hasa vijana na kina mama kutokengeuka mara baada ya kupokea mikopo na kuwataka kusimamia malengo ya vikundi.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo aliiagiza ofisi ya maendeleo ya jamii kuendelea kutoa elimu ya biashara kwa wajasiliamali ili wanapopata mikopo waitumie kwa tija huku akiwataka wanufaika wa mikopo kukata bima ya afya.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *