Hamas yakosoa pendekezo la Trump kuichukua Gaza

PALESTINA : MATAMSHI ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu pendekezo la Marekani kuchukua udhibiti wa Gaza yamekosolewa vikali na kundi la Hamas, ambalo limeyaita matamshi hayo kuwa “ya chuki” na “hatari kwa utulivu wa kikanda.”

Katika taarifa yake ya Jumanne, Hamas limesema, “Matamshi kama haya ni ya chuki kwa watu wetu na maadili yetu, na hayatasaidia katika utulivu wa kikanda.

“Tunatoa wito kwa utawala wa Marekani na Rais Trump kuachana na matamshi haya ya kutowajibika, ambayo yanakinzana na sheria za kimataifa na haki za kimsingi za watu wetu wa Palestina katika ardhi yao.”

Kundi hilo pia limesema linatoa wito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa kuandaa mikutano ya dharura ili kushughulikia matamshi hayo na kuchukua msimamo mkali kulinda haki za Wapalestina.

Matamshi ya Rais Trump yalikuja baada ya mkutano wake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambapo Trump alidai kwamba Marekani inaweza kuchukua udhibiti wa Gaza na kuwahamisha Wapalestina milioni 1.8 walioko katika eneo hilo kwenda nchi nyingine za Kiarabu.

Trump aliongeza kuwa, baada ya Marekani kuijenga upya Gaza, eneo hilo linaweza kuwa makazi ya “watu wa dunia nzima.” SOMA: Marekani yajipanga kuchukua udhibiti Gaza

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button