MAREKANI : RAIS wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani itachukua udhibiti wa eneo la Gaza, ikiwa itafanikiwa kuimiliki.
Kauli hiyo aliitoa wakati alipozungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Jumanne, kwa ajili ya mazungumzo muhimu kuhusu usitishaji wa mapigano na wanamgambo wa Hamas.
Taarifa zinasema kuwa endapo Marekani itafanikiwa kutawala Gaza, hatua hiyo itakuwa inavunja sera ya miongo kadhaa ya Marekani kuhusu mzozo wa Israel na Palestina.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano na Netanyahu, Trump alisema kuwa Wapalestina wanastahili kuondoka Gaza, eneo lililoharibiwa kwa vita, na kuhamia katika nchi nyingine za Mashariki ya Kati kama Misri na Jordan.
Trump alieleza kuwa Marekani ina mpango wa kuisafisha Gaza kwa kuondoa mabomu yasiyolipuka, na kuanzisha ustawi wa kiuchumi utakaohusisha ajira na makazi kwa watu watakaohamia katika eneo hilo.
Rais huyo aliongeza kuwa kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kuwaondoa Wapalestina kutoka Gaza, atafanya ziara katika maeneo ya Gaza, Saudi Arabia, na Israel, ingawa hakuweka wazi ratiba ya ziara hiyo.
Hatua ya kuwalazimisha Wapalestina kuondoka Gaza inaweza kuwa kinyume cha sheria za kimataifa na inaweza kukutana na upinzani mkali kutoka Mashariki ya Kati na kutoka kwa marafiki wa Marekani Magharibi.
Baada ya kikao hicho, Saudi Arabia ilitoa tamko ikisisitiza kukataa hatua ya kuwaondoa Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Netanyahu alimsifu Trump kama “rafiki mkubwa zaidi” wa Israel, akisema mpango wa Trump kwa Gaza unaweza kubadili historia na ni jambo linalostahili kuangaliwa kwa karibu.
Mbali na hayo, Trump alieleza kuwa anapenda kuingia katika makubaliano na Iran ili kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo, lakini aliongeza kuwa hilo linahitaji Iran kuacha kuunda silaha za nyuklia.
Kuhusu vita vinavyoendelea nchini Ukraine, Trump alisema utawala wake unaendelea kufanya mazungumzo na Urusi na Ukraine, na mazungumzo hayo yanaendelea vyema.
Netanyahu alikua kiongozi wa kwanza wa kigeni kufanya ziara katika White House tangu Trump aingie madarakani takribani wiki mbili zilizopita.