Handeni Mji kuzindua Jukwaa uwezeshaji wanawake

TANGA; KUELEKEA kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Halmashauri ya Mji Handeni inatarajia kuzindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambalo litawaimarisha katika shughuli zao za kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo ambayo yatafanyika Machi 7, 2026 kwa Handeni Mji, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amesema uzinduzi huo utafanyika kesho katika kongamano la wanawake ambalo linalolenga kuwaunganisha wanawake ili kubadilishana uzoefu, kupata taarifa za fursa za kiuchumi na kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali.
Amesema halmashauri hiyo inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Kongamano hili pia litaambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wanawake wajasiriamali, ili kuonesha ubunifu wao pamoja na juhudi wanazofanya katika kujikwamua kiuchumi,”amesema.
Ameongeza kuwa katika kongamano hilo washiriki watapatiwa elimu mbalimbali ikiwemo masuala ya umiliki wa ardhi na mirathi, malezi na makuzi ya watoto, ujasiriamali na biashara, elimu ya ushirika na SACCOS pamoja na kilimo bora na ufugaji wa kisasa.



