Harakisheni mchakato wa sheria – Mchengerwa
Ataka huduma iende kwenye majiji

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ameuelekeza Uongozi wa Wakala wa Mabasi ya Mwendokasi (DART) kuharakisha mchakato wa marekebisho ya sheria ili mabasi hayo yaweze kufika maeneo mengi zaidi.
Mchengerwa ameyasema hayo kwenye ziara yake kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART)
Amesema, sheria iliyopo sasa inamnyima wakala kufika baadhi ya maeneo akitolea mfano Mbagala mpaka Mkuranga.
“Fanyeni haraka turekebishe sheria ili mabasi yafike hadi Mkuranga, hayo ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan. ” Amesema na kuongeza

“Gongolamboto mpaka Pungu na njia panda ya Kisarawe, Chanika, Chamazi, Mbagala rangi tatu, Kongowe hadi Mkuranga.
Amesema pia, yafike mpakani mwa Bagamoyo, Tabata na upanuzi wa barabara Kimara hadi Kibaha.
“Tunataka huduma iende Dodoma lakini kwanza tujiulize huduma zetu zinawafurahisha wakazi wa Dar es Salaam? alihoji Mchengerwa
“Tunataka kutanua mtandao kwa jiji la Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza, lakini lazima tujiridhishe utolewaji wa huduma inayotolewa Dar es Salaam inamfurahisha kila Tanzania anayeishi Dar es Salaam na mtumiaji wa mwendokasi?
Amesema, idadi ya watanzania wanaotumia Mwendokasi imeongezeka kutoka 90,000 hadi 200,00
“Suala la utoaji huduma Dar es Salaam halina mjadala, kuanzia sasa mjirekebishe, sitaki kusikia wananchi wanalalamika, nikisikia tu nachukua hatua.
“Mimi ni mtu wa maamuzi, nikidhibitisha Afisa kazembea nakula kichwa.” Amesema



