KAMA ulifikiria Hasheem Thabeet amestaafu kikapu mwenyewe anakwambia bado yupo sana na ataendelea kukipiga mpaka pale atakapoamua kutangaza mwenyewe mwisho wa kucheza.
Akizungumza na Dailynews digital Dar es Salaam Thabeet amesema baada ya mwaka uliopita kurudi Dar es Salaam na kucheza klabu ya Pazi amerejea tena kimataifa na sasa atakuwa Taiwan msimu huu.
Amesema hapendi kusema ni lini atastaafu kwani bado anaamini ana uwezo wa kucheza na kufanya vizuri.
SOMA: JMK Park, ICARRe kuibua vipaji kikapu
“Sifikirii habari za kustaafu kwa sasa, nipo naendelea kucheza wakati ukifika nitasema, “amesema na kuongeza kuwa kwa sasa anacheza Kaohsiung 17LIVE Steelers ya Taiwan.
Kabla ya kurejea Pazi, alikuwa Taiwan Herobears na Sichuan Blue Whales.
Amesema mpango wake hapo baadaye kama akistaafu anafikiria kuwasaidia vijana wenzake kufikia ndoto kama zake za kukipiga nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Thabeet, kuna wachezaji kadhaa walimfuata na kumuomba awasaidie wacheze kikapu ya kulipwa nje na hilo anaendelea kulifanyia kazi.
Nyota huyo amewahi kucheza klabu mbalimbali Marekani, China, Japani na Taiwan zikiwemo Memphis Grizzlies, Dakota Wiz, Houston Rockets, Yokohama B Corsairs na Hsinchu JKO Lioneers.