Hati 40 zatolewa Samia Ardhi Kliniki

ARUSHA: NDANI ya siku mbili Ofisi ya Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Arusha imefanikiwa kutoa hati 40 katika siku saba za ”Samia Ardhi Kliniki” iliyoanza marchi 2 mwaka huu.
Katika Kliniki hiyo ambayo inatarajia kumalizika Machi 7 mwaka huu, wananchi 117 wamepokelewa na kusikilizwa changamoto zao za ardhi na kutatuliwa katika kliniki hiyo.

Kwa Mujibu, Kamishina Msaidizi wa Ardhi mkoani Arusha, Frank Minzikuntwe amewaomba wananchi wenye uhitaji wa hati kuchangamkia fursa hiyo ya kliniki ili waweze kuhudumiwa kwani kasi iliyopo ni ndogo sana na wao wamejipanga kumaliza changamoto za utoaji wa hati na migogoro ya ardhi kwa wakazi Arusha.
Minzikuntwe alisema kuwa ofisi zake zote zimehamishiwa katika uwanja wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha kusikiliza kero za migogoro ya ardhi na kuitatua na pia kuhakikisha wale wote waliopeleka maombi ya uhitaji wa hati wanapata huduma hiyo kwa muda mfupi kwa kuwa maofisa wote wako katika eneo moja.

Alisema wenye maombi ya zamani na ya sasa ya uhitaji wa hati yanafanyiwa kazi kwa uharaka katika Kliniki hiyo lengo ni kutaka kila mmoja kuwa na hati iliyoingizwa kwenye mfumo ili ulipaji kodi ya ardhi uweze kutambulika kirahisi.
Kamishina alisema kuwa Rais amekuwa akisisitiza mara kwa mara utoaji wa hati usiwe na usumbufu na ofisi za ardhi zitatue migogoro ya ardhi kwa wananchi na Kliniki ya ‘’Samia Ardhi Kliniki’’ ni mworobaini wa kila kitu hivyo aliwaomba wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa faida yao.
Akizungumzia migogoro waliyokutana nayo katika siku tatu za Kliniki ya ‘’Samia Ardhi Kliniki’’ ni pamoja na migogoro ya mirathi na watu kudhurumiana ardhi na wamekuwa wakijitahidi kukutanisha pande zote na hatimaye kutatua changamoto hizo na kwa kiasi kikubwa wameweze kufanikiwa kwa hilo.

‘’Nawaomba wananchi wa jiji la Arusha na mkoa kwa ujumla kuchangamkia Samia Ardhi Kliniki kupata hati na kutatua migogoro yao ya ardhi kwani wiki moja sio nyingi kila mmoja afanye hivyo kwa maslahi yake na serikali kwa ujumla’’alisema Kamishina
Naye, mkazi wa kata ya Muriet aliyejitambulisha kwa jina la Masoud Laizer ameishukuru Kliniki hiyo kwani amepata hati yake kwa muda mfupi baada ya kuwasilisha nyaraka zote zinazohitajika kwa ajili ya upatikanaji wa hati.
Mkazi mwingine wa kata ya Daraja Mbili,Ally Juma yeye alisema alisumbuka kwa muda mrefu kuisaka hiyo hati lakini ujio wa Kliniki umeifanya yeye kuifuatilia na kuipata na kuishukuru serikali kwa uamuzi huo ambao alisema uwe unafanywa mara kwa mara.



