Hati fungani ya NMB yatuzwa kimataifa

HATI fungani ya NMB Jasiri ya Benki ya NMB imechaguliwa kuwa mshindi wa kwanza wa tuzo mpya ya Hati Fungani Endelevu ya Mwaka iliyoanzishwa kimataifa kutunuku taasisi zilizofanya vizuri eneo hilo.

Waandaaji wa Tuzo za Kimataifa za Mitaji kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, kwa kushirikiana na nchi tajiri kwa viwanda duniani (G20), Shirika la IFC (Mwanachama wa Benki ya Dunia) pamoja na Jukwaa la Kufadhili Ujasiriamali (SME Finance Forum), ndio walianzisha kipengele hicho mwaka huu.

Ushindi huo wa NMB Jasiri umepatikana baada ya Hati Fungani hiyo kupitiwa na jopo la majaji zaidi ya 100 waliovutiwa na mlengo wake, muundo na uwezo wa kulihudumia kifedha kundi ambalo halizingatiwi kwa mitaji ya kawaida iliyozoeleka.

Chanzo hiki cha mtaji kinaendana vyema na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na Kanuni za Dhamana za Kijamii za Chama cha Kimataifa cha Masoko ya Mitaji.

Katika hotuba yake ya kukubali tuzo na heshima hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema “Sisi NMB tumejitolea kuhakikisha tasnia ya fedha inachangia maendeleo ya Tanzania. Hati Fungani ya Jasiri yenye lengo la kupunguza pengo la mitaji linalozikabili biashara ndogo ndogo na za kati zinazomilikiwa au kusimamiwa na akinamama ni keielelezo kizuri cha dhamira hii.”

“Hati Fungani yetu imefanikiwa kupata matokeo yaliyotarajiwa ya kusaidia kuwawezesha wanawake kiuchumi na kushughulikia madhumuni matatu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo ni lengo la kwanza, la tano na la kumi,” alisema Zaipuna katika taarifa iliyotolewa jana na benki hiyo.

“Tuzo hii ni wakati muafaka wa kihistoria kwa sekta ya benki nchini, kwani inaiweka nchi yetu katika ramani ya dunia kwa uongozi kwenye mitaji endelevu. Hati Fungani ya Jasiri inaweka kigezo kipya nchini na barani Afrika katika kukuza vyanzo vingine vya mitaji mbadala kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa kimataifa,” aliongeza.

Zaipuna alisema tuzo hiyo ni kwa ajili wa wafanyakazi wote wa NMB, washirika wake, wawekezaji na wasimamizi wa sekta ya fedha kwa kuchangia mafanikio makubwa ya dhamana ya Jasiri.

Tuzo hiyo imetolewa Phnom Penh nchini Cambodia jana.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button