KAMA Tanzania ingekuwa kampuni iliyosajiliwa katika soko la hisa, wiki iliyopita hisa zake zingepanda. Katika masoko yote makubwa ya hisa duniani yakiwamo ya London na New York, hisa za kampuni za Shell, Equinor na Exxon Mobil, ziliongezeka thamani.
Kilichosababisha kupanda kwa bei ya hisa hizo kilikuwa ni kufikiwa kwa makubaliano baina ya kampuni hizo na Serikali ya Tanzania kuhusu kuanza kwa mradi wa kuzalisha gesi iliyosindikwa (LNG) mkoani Lindi.
Habari hii ilikuwa njema kwenye masoko ya hisa na duniani kwa ujumla kwa sababu kubwa mbili; Mosi ni ukweli kwamba vita ya Urusi na Ukraine imesababisha mahitaji makubwa ya gesi kwa vile nchi nyingi za Ulaya zilikuwa zinategemea gesi kutoka Urusi ambayo sasa wameiwekea vikwazo vya kutofanya nayo biashara.
Pili ni ukweli kwamba mazungumzo hayo ya Tanzania yalionekana kukwama kabisa kuanzia mwaka 2016 hadi alipoingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Machi mwaka 2021.
Kwa hiyo kukubaliana huko kati ya Tanzania na kampuni hizo za kimataifa kulimaanisha uwezekano wa kupata gesi ya uhakika na kwa wingi Tanzania ikiwa na akiba ya mita za ujazo trilioni 57.54, lakini kubwa zaidi ni kwamba wamepata kufanya biashara na nchi yenye amani, kutabirika na kwenye uhakika wa kufaidika kwa pande zote mbili, kwa maana ya mwenye mali na wawekezaji.
Ilikuwaje mradi huu mkubwa kuliko yote kwenye historia ya Tanzania na unaotajwa kuwa na thamani ya dola bilioni 42, ukaweza kurudi mezani na kufikia hatua hii wakati miaka michache iliyopita, mabosi wa kampuni hizo walianza kuzungumzia uwezekano wa kuachana nao?
Kuna watu wawili wanastahili kutajwa na kupewa ‘maua’ yao kutokana na hatua iliyofikiwa sasa; Rais Samia na Waziri wa Nishati, January Makamba.
Makala haya yatajikita zaidi kwa Waziri January Makamba kwa sababu mbili za majukumu alilopewa na pia muktadha wa kisiasa nchini wakati huu.
Wakati Rais Samia alipokuwa akimwapisha January mnamo Septemba 2021, alimpa maelekezo mahususi ya kuhakikisha suala la mradi huu linarejea mezani na kukamilika haraka iwezekanavyo kwa maslahi ya taifa.
Ingawa mradi huu ulibuniwa na mchakato kuanza wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ulipoteza nguvu enzi za utawala wa hayati Rais John Magufuli.
Hali ilikuwa mbaya zaidi Januari mwaka 2021 wakati mmoja wa wawekezaji wakubwa zaidi kwenye mradi huo, kampuni ya Equinor ya Norway ilipotangaza kufuta uwekezaji wa kiasi cha dola milioni 982 ilichopanga kutumia katika hatua za awali, ikidai kwamba mradi huo hauna faida tena kwao kutokana na mabadiliko ya kisheria na kutotabirika kwa sera za uwekezaji za Tanzania wakati wa utawala wa Rais Magufuli.
Kabla January hajateuliwa kuwa Waziri wa Nishati, tayari Rais Samia alishawaita wawekezaji mezani na kukubaliana kurejea katika majadiliano na makubaliano ya uwekezaji huo tangu Juni 2021. Ni mzigo huo ambao Rais Samia aliamua kumtwisha January alipompa wadhifa huo na kumpa maelekezo hayo kwa utekelezaji.
Kuelewa kazi kubwa iliyofanywa na January na wenzake kwenye wizara hiyo ni kuelewa kile ambacho wachumi na wataalamu wa masuala ya uwekezaji hukiita Lucas paradox. Mchumi mmoja wa Marekani, Robert Lucas, ndiye aliyebuni dhana hiyo – akieleza kwa nini si rahisi kwa mitaji kutoka mataifa tajiri kupelekwa mataifa masikini ingawa yana utajiri wa nguvu kazi na maliasili.
Kwa kanuni za kawaida za kiuchumi, ilitakiwa iwe rahisi kwa mitaji kutoka Ulaya, Asia na Marekani kuja Afrika kuliko na madini, mafuta, gesi na kundi kubwa la nguvukazi ya vijana. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa mitaji hubaki hukohuko na Afrika kupata kiduchu. Hiyo ndiyo Lucas paradox na kazi aliyopewa January na Rais ilikuwa ni ya kukinzana na dhana hiyo.
Kwa nini kuna Lucas paradox? Ni kwa sababu nchi nyingi za Afrika zina shida za kiulinzi na kisalama, zina mazingira yasiyo rafiki kwa wawekezaji, zina sera zisizotabirika (kwa maana ya kubadilikabadilika kutokana na maono ya walio madarakani, ukosefu wa rasilimali watu ya kutosha kwa kazi za kitaalamu, ukosefu wa teknolojia za kisasa barani Afrika na mambo mengine.
Kwa kifupi, January alitakiwa kufanya kazi ya kuwashawishi wawekezaji warejee mezani kuzungumzia mradi mkubwa zaidi wa uwekezaji Mashariki na Kusini mwa Afrika kwenye sekta hiyo; akitoka katika chama na serikali ileile iliyowabadilikia miaka michache tu iliyopita.
Na kampuni zinazokwenda Lindi hazitoki kwenye nchi moja. Kila nchi ina maslahi yake binafsi, mahitaji yake binafsi na sera na taratibu zake kuhusu namna ya kurejea mezani kuzungumza na nchi – ya Afrika, iliyokiuka yenyewe mazungumzo mliyokuwa mmekubaliana awali. Kazi ilikuwa ni kuzungumza na kuanzia mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa, mawaziri wa nchi zao wa masuala ya nishati, wakuu wa kampuni husika na wakati mwingine kupitia viongozi wa nchi zinazotoka kampuni hizo
Hatua tuliyofikia sasa ni hatua tuliyopaswa kuwa tumefikia mwaka 2019 kama isingekuwa mabadiliko ya kiutawala na kisheria yaliyofuata Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Ni kupitia safari kadhaa kwenye nchi husika, kuonyesha mwenendo na tabia zinazoonesha kufanya unachozungumza na kuanza kutabirika kwa utawala wa Rais Samia. Lakini, mtu aliyekuwa akilala na kuamka kuhakikisha jambo hili walau linafikia hapa ni January.
January kwa bahati mbaya, amefanya kile ambacho Profesa Sospeter Muhongo alikifanya wakati alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini kwenye utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Si Watanzania wengi wanajua lakini ni Muhongo ndiye aliyepambana zaidi kuhakikisha kwamba mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania unapitia nchini kwake.
Watu wengi wanafahamu kwamba kuna wakati ilikuwa nusura mradi ule uwe ni kati ya Uganda na Kenya. Nafahamu si watu wengi wanaofahamu kwamba ni Muhongo, kwa baraka za Kikwete, ndiye aliyeishawishi Uganda na kuhakikisha inapata kila ilichokitaka, ili Tanzania ipate fursa ya kupitisha bomba hilo na si jirani zake hao. Kama ilivyo kwa January leo, Watanzania wanafurahia bomba la mafuta kupita Tanzania lakini ni wachache wanaojua huenda isingekuwa hivyo pasipo juhudi binafsi na umahiri wa Muhongo.
Wizara ya Nishati ni ngumu
Katika historia ya Tanzania huru, ni wanasiasa wachache sana wamedumu katika nafasi ya Waziri wa Nishati kwa walau muhula mmoja wa urais yaani miaka mitano. Kimsingi, ukimuondoa Al Noor Kassum aliyeongoza wizara hiyo kwa nyakati tofauti enzi za utawala wa marais Julius Nyerere na Ali Hassan Mwinyi, wastani wa mawaziri ni chini ya miaka mitatu. Hii ni wizara inayobeba maslahi ya wengi na mara kadhaa imegeuka kuwa ‘kaburi’ la wanasiasa.
Katika kipindi cha miaka 10 ya Kikwete, wanasiasa mashuhuri kama Nazir Karamagi, Dk Ibrahim Msabaha, William Ngeleja na Muhongo walihudumu kwenye wizara hiyo na hakuna aliyeondoka kwa heshima kubwa. Karamagi aliondolewa kwa kashfa ya Buzwagi, Msabaha kwa Sakata la Richmond, Ngeleja kwenye mabadiliko ya baraza la mawaziri ya mwaka 2012 na Muhongo kwa suala la kampuni ya kufua umeme ya IPTL kupitia sakata lililojulikana kwa jina la Escrow.
Wakati January alipopewa wadhifa huo na Samia, wapo waliofurahia wakiamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake kisiasa. Baadhi ya rafiki zake walimpa pole kwa kupewa wizara ambayo wanaopewa wadhifa huo huwa wana nafasi kubwa ya kushindwa kuliko kufanikisha ndoto zao.
January ana historia ya nyuma na mradi huo. Wakati akiwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira enzi za Magufuli, alizungumza hadharani umuhimu wa kufanya upembuzi yakinifu wa kimazingira kuhusu mradi huo. Hii ilitokana na ukweli kuwa zipo taasisi za kimataifa zilizosema mradi utakuwa na athari za kimazingira.
Wakati January anapewa wizara hiyo, mradi ulikuwa umekamilika kwa chini ya asilimia 40. Nilipotembelea mradi huo mwezi uliopita, ulikuwa umeendelea kufikia takribani asilimia 85. Hii maana yake ni kwamba ndani ya miaka miwili ya utawala wa Rais Samia, kasi ya ujenzi imekuwa takribani mara mbili ya kasi iliyokuwepo kwenye miaka mitano ya mtangulizi wake. Hii ni spidi ya kipindi cha utawala wa Samia lakini January ndiye waziri na msimamizi wa jambo hili. Kama angekuwa mwanasiasa mwenye kinyongo au kuangalia maslahi binafsi kuliko ya nchi, huenda asingefanya jitihada alizofanya kuhakikisha mradi unaendelea.
Haijulikani na wengi lakini ninafahamu kwamba kazi ya kufanya mradi wa Bwawa la Nyerere ufike ulipo sasa ilikuwa ngumu; ikihusisha mazungumzo ya mara kwa mara na Rais Abdel Fatah al Sisi wa Misri ambayo ni wadau muhimu kwenye mradi huo pamoja na taasisi kadhaa za kifedha za kimataifa. Hili ni eneo lingine ambalo waziri huyu wa nishati ametimiza wajibu wake ipasavyo.
‘Dude’ liitwalo Tanesco
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ni miongoni mwa mashirika ya umma makubwa zaidi hapa Tanzania. Ukitaka kujua ukubwa wa taasisi hii tazama idadi ya wafanyakazi wake wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 10,000. Ni shirika kubwa na lililoenea nchi nzima ingawa matatizo ya umeme hayajawahi kuondoka hapa nchini.
Nini ambacho January amefanya Tanesco?
Kuna mambo makubwa matatu ambayo ameyafanya hadi sasa kwa mtazamo wangu. Kwanza, alipendekeza wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka katika kada ambayo haikuwa imezoeleka huko nyuma. Maingizo ya wajumbe wa aina ya Abubakar Bakhresa, Nehemia Mchechu na Christopher Gachuma, yalikuwa na lengo la kuingiza mawazo mapya na watu ambao wana maslahi na umeme wa uhakika hapa nchini.
Jambo la pili lilikuwa ni pendekezo la wizara yake kwa serikali kwamba ichukue madeni yote ya nyuma ambayo Tanesco ilikuwa ikidaiwa na serikali kutokana na huduma tofauti za huko nyuma. Serikali ya Rais Samia ilikubali pendekezo hilo na hilo maana yake ni kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka ya karibuni, hesabu za shirika hilo hazitakuwa na hasara.
Kwa hesabu za Tanesco kutokuwa na hasara inamaanisha itaaminika kwa wadau wa sekta hiyo na kuanza kujiendesha kwa faida. Badala ya kulipa madeni makubwa ambayo wakati mwingine yalionekana kama hayalipiki, Tanesco sasa ingetumia mapato yake kufanya shughuli zitakazoboresha huduma kwa wateja wake.
Jambo la tatu linahusu huduma. Kwa watu wanaotumia huduma za Tanesco, watabaini kwamba katika siku za karibuni wateja huhudumiwa kwa haraka zaidi na watoa huduma kuliko ilivyokuwa nyuma na shirika limeanza jitihada za makusudi kuboresha miundombinu yake ya kuzalisha umeme.
Katika mkutano uliofanyika wiki iliyopita kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande na wahariri wa vyombo vya habari hapa nchini, wahariri walizungumzia suala la kuimarika kwa suala zima la huduma kwa wateja ambapo sasa waliopiga simu kutaka huduma walipata majibu kwa wakati na shida zao kutekelezwa.
Bado umeme umekuwa ukikatika na kuleta kero kwa wananchi lakini January amezungumza hadharani kuwa pamoja na mambo mengine, uchakavu na kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kwa miundombinu ya kuzalisha na kusambaza umeme imekuwa ni tatizo kubwa.
Kwa wajuvi wa masuala ya umeme, hii ni sababu yenye mashiko. Taifa la Afrika Kusini linazalisha umeme mwingi kuliko mahitaji yake lakini kwa sasa linakabiliwa na mgawo wa umeme kwa saa hadi 10 kwa siku. Wataalamu wa ‘Tanesco’ ya Afrika Kusini, Eskom, wanataja suala la ukosefu wa uwekezaji kwenye mitambo na uchakavu wa miundombinu kama mojawapo ya sehemu ya tatizo.
Unaona kwamba kama Tanesco itaanza kutumia mapato yake kununua mitambo mipya na kufanya ukarabati wa ile iliyochakaa huku kiwango cha uzalishaji kikipanda, tatizo la kukatika kwa umeme linaweza kupungua kwa kadri miaka inavyokwenda.
Muda utatoa hukumu sahihi
Katika moja ya hotuba zake bungeni mwaka jana, January aliwaomba wabunge wampe muda wa kutekeleza majukumu aliyopewa na Rais Samia na kwa picha kubwa zaidi, Watanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichopewa idhini ya kutawala nchi kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2020.
Bahati nzuri ni kwamba tabia ya wizara yenyewe aliyopo January ni kuwa haikawii ‘kumtapika’ isiyemtaka na kuwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ni mawaziri wawili tu; Ngeleja na Dk Medard Kalemani ndiyo waliokaa madarakani kwa zaidi ya miaka mitatu. Kwa yote ambayo mtoto huyu mkubwa wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuph Makamba, amekuwa akihusishwa nayo, ameweza kuvuka vigingi vya Bwawa la Nyerere, LNG ya Lindi na Tanesco kwa maksi za juu.
Kila wakati kumekuwa na maneno ya mwanasiasa huyu kuwa na ukwasi usio wa kawaida na maneno mengine yanayohusiana na hayo lakini hadi sasa hakujawahi kutokea ushahidi wa aina yoyote kuthibitisha madai dhidi yake ambayo yamedumu kwa zaidi ya muongo mmoja tangu ajitose rasmi katika siasa mwaka 2010. Kilichopo mara zote ni maneno yasiyo na ushahidi wa maandishi au mali alizonazo.
Pamoja na yote yanayosemwa juu yake, vitu vichache vina ushahidi kumhusu; kwamba alikuwa mmoja wa wabunge mahiri kiasi cha kuongoza Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika kipindi chake cha kwanza bungeni mwaka 2010, alikuwa mmoja wa vinara wa kampeni za CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uliomwingiza madarakani Magufuli, na katika muda wa chini ya miaka miwili tangu ateuliwe kuwa waziri, ameirudisha wizara ya nishati kwenye chati.
Mradi wa Bwawa la Nyerere unaendelea kwa kasi zaidi, mradi mkubwa kuliko yote kwenye historia ya Tanzania wenye thamani sawa na nusu ya Pato la Taifa (GDP) unaelekea kuanza kutekelezwa Kusini mwa taifa letu baada ya miaka kadhaa ya kusuasua, na kesho ya Tanesco ina matumaini kuliko ilivyokuwa jana na leo.
Nadhani hatumtendei haki January Makamba.