LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo mitatu ikipigwa viwanja tofauti.
Katika mchezo wa mapema ‘Wachimba dhahabu’ wa Chunya, Ken Gold itakuwa wenyeji wa ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Coastal ipo nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 12 baada ya michezo 11 wakati Ken Gold inashika nafasi ya 16 mwisho wa msimamo ikiwa na pointi 5.
Kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, ‘Wauaji wa Kusini’, Namungo itakuwa mgeni wa ‘Wanamapigo na Mwendo’, Mashujaa.
Mashujaa ni ya nane ikiwa na pointi 13 baada ya michezo 11 wakati Namungo ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi tisa baada ya michezo 10.
Mkoani Dar es Salaam, ‘Wanalambalamba’, Azam itakuwa mwenyeji wa ‘Walima Miwa’, Kagera Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi.
Azam ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 21 baada ya michezo 10 wakati Kagera Sugar ni ya 14 ikiwa na pointi nane.