HIVI karibuni bungeni Dodoma, serikali kupitia Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, imeelekeza wachambuzi kwenye vyombo mbalimbali vya habari kusoma walau kozi fupi za michezo.
Mwinjuma alitoa maagizo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaka kujua serikali ina mpango gani kuhusu upotoshaji wa habari za michezo unaofanywa na wachambuzi kwenye vituo hivyo.
Mwinjuma alisema ingawa wachambuzi hawapendi kulisikia jambo hilo, lakini lipo kwa mujibu wa sheria.
Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, kifungu cha 19 (1) inasema watu wote wanaotaka kufanya
uchambuzi kwenye vyombo vya habari lazima wasome kozi fupi za michezo.
Tunaunga mkono kauli hii ya Naibu Waziri Mwinjuma kwa sababu mbali ya kuwa ipo kisheria, lakini ni muhimu kwa maendeleo ya michezo yenyewe.
Kwanza, kama wachambuzi watakuwa na elimu ya michezo mbalimbali, wataweza kuichambua kwa marefu na mapana na kuiongeza ufahamu kwa tabaka la watu wote hasa kizazi kijacho.
Kwa mwendo wanaokwenda nao wachambuzi wengi kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni, ni wazi hawasaidii kwa kiwango kinachotakiwa ukuaji wa michezo yenyewe zaidi ya kufanya hivyo kwa hisia na utashi binafsi na si uelewa unaotaka na kupata elimu ya michezo.
Michezo ni moja ya maeneo yanayotoa ajira nyingi rasmi na zisizo rasmi kwa Watanzania wa rika lote.
Hivyo kama wachambuzi wanaofuatiliwa kwa kiwango kikubwa kupitia vyombo vya habari watakuwa na elimu,
wanaweza kufanya kwa weledi chambuzi zao na kuvutia watu wengi. Kuanzia utawala, waamuzi, makocha na wachezaji wa michezo yenyewe, wachambuzi wanahitaji kuwa na elimu kuweza kutendea haki kila eneo katika haya tuliyoyainisha.
Ni matamanio yetu kuona mchambuzi anachambua mambo ya kiutawala kwenye mpira wa miguu au mchezo mwingine wowote basi afanye hivyo kwa upana wake.
Kadhalika, wakichambua mambo ya waamuzi, wachezaji, mikataba na mambo mbalimbali yanayohusu sheria, maadili michezoni wafanye kwa weledi mkubwa unaotokana na elimu ya michezo.
Tuliwahi kumsikia Rais wa Shirikisho la Soka (TFF) siku moja akisisitiza umuhimu wa wachambuzi kufanya kazi zao
kwa weledi na sio kuzusha taharuki na migogoro ambayo kwa namna moja au nyingine haiwezi kusaidia ukuaji wa michezo yenyewe.
Kwa nchi zilizoendelea, uchambuzi wa masuala ya michezo unafanywa zaidi na watu waliowahi kucheza kwa kiwango cha juu michezo hiyo.
Inawasaidia kufanya uchambuzi wao kwa mawanda mapana na kutengeneza imani kwa wanaofuatilia.
Hata hivyo, hili ni tofauti sana hapa nchini na ndiyo maana ikawekwa hiyo sheria inayowataka wachambuzi kurudi shule kupata elimu ya michezo mbalimbali kabla ya kufanya kazi hiyo.