MATUMIZI ya muda mrefu ya baadhi ya vyakula, hasa mihogo na karanga, vyenye sumukuvu yanasababisha homa ya ini.
Kwa mujibu wa machapisho mbalimbali, kuvu ni sumu zitokanazo na aina ya ukungu (fangasi) unaoota kwenye mbegu za nafaka na jamii ya kunde pamoja na mazao ya mizizi, ikiwemo mihogo na karanga. Sumukuvu zinaweza kushambulia mmea wenyewe ukiwa bado shambani au mazao wakati mavuno, hasa uhifadhi (mazao) unapokua hafifu.
Sumu hizo hujikusanya taratibu katika mwili wa binadamu kwa muda wa miaka kadhaa na kwenda moja kwa moja kuathiri ini.
Wakati athari za sumukuvu katika mihogo na karanga zinachukua muda mrefu kuonekana kwa watu wazima, takribani miaka minne au mitano, kwa watoto zinaonekana mapema, pengine hata ndani ya mwaka, ambapo mbali na kuharibu ini zinawasababishia udumavu.
Kwa watu wazima, athari za sumu kwa ini zina matokeo sawa na matumizi ya pombe kwa kiasi kikubwa pamoja na dawa za hospitali bila maelekezo ya wataalamu.
“Matumizi ya sigara ni chanzo cha tatizo pia,” anasema Mtaalamu wa Afya Kitengo cha Magonjwa ya Ndani Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dickson Phillemon, wakati wa siku ya afya, maarufu ‘Afya Day’ katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza.
Bugando imeshiriki sherehe hizo kwa kutoa huduma za baadhi ya vipimo na ushauri bure kwa wanafunzi na watumishi wa kampasi, pamoja na jamii inayozunguka taasisi hiyo.
Dk Phillemon anaelimisha zaidi kwamba mbali na baadhi ya aina za vyakula, majimaji yoyote yanayotoka katika mwili wa binadamu mwenye dalili ya homa ya ini, kama vile mate, jasho na damu yasiguswe kwa sababu ni moja ya vyanzo vikuu vya maambukizi ya ugonjwa huo.
Licha ya uwepo wa aina tano (A, B, C, D na E) za homa ya ini, chanjo inatolewa kwa aina ya pili tu, na inaziwakilisha aina zingine zote.
Chanjo ya kwanza inatolewa mara tu baada ya mtu kufanya vipimo na kugundulika hana virusi vya homa ya ini, ya pili ni baada ya mwezi mmoja na ya tatu baada ya miezi sita. Baada ya hapo chanjo itadumu katika mwili wa binadamu kwa miaka 10.
Baada ya kipindi hicho mtu atalazimika kuchoma kichocheo (booster) cha chanjo hiyo, iweze kufanya kazi maisha yake yote. Baadhi ya dalili za homa ya ini ni pamoja na rangi ya macho na ngozi kuwa njano, maumivu ya tumbo upande wa kulia lilipo ini, maumivu ya misuli, kichefuchefu na kupungua uzito.
Dk Phillemon anawasisitiza wanajamii kupima na kupata chanjo ya homa ya ini, kwa sababu ugonjwa huo bado haujapata matibabu ya moja kwa moja.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara ya Afya katika maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini duniani, Julai 28 mwaka jana, inasema aina ya virusi vya homa ya ini A na E huambukizwa kwa njia ya kunywa maji na chakula kisichokuwa salama kwa kuchafuliwa na kinyesi chenye maambukizi ya virusi hivyo, ambapo dalili zake zinafanana kwa kiasi kikubwa na uambukizwaji wa magonjwa ya kuhara.
Kadhalika taarifa inasema kwamba virusi aina B, C na D huambukizwa kwa njia sawa na za magonjwa ya ngono na Virusi vya Ukimwi (VVU) kama vile kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana, utumiaji usio salama wa sindano na kujichoma na vitu vyenye ncha kali, majimaji ya mgonjwa kumpata mtu mwingine kama ana kidonda, na pia mama anaweza kumwambukiza mtoto wake wakati wa kujifungua.
“Aina ya homa ya ini inayosababishwa na virusi vya kundi B yaani Hepatitis B (HBV), ndiyo inayoongoza kwa maambukizi nchini,” inasema taarifa hiyo na kuongeza kwamba: Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia taarifa ya homa ya ini ya mwaka 2021, zinaonesha mwaka 2019 watu milioni 296 duniani walikuwa wanaishi na homa sugu ya ini aina ya B, ambapo zaidi ya nusu (asilimia 66) ya maambukizi hayo yalikuwa yanatoka Afrika.
Aidha, watu wapatao milioni 58 walikuwa wanaishi na maambukizi ya homa sugu ya ini aina C na kulikuwa na vifo 820,000 duniani kutokana na homa ya ini aina B. Kwa Tanzania, takwimu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) zinaonesha maambukizi ya homa ya ini aina B miongoni mwa wachangiaji damu kwa miaka mitatu ni asilimia 4.4 mwaka 2018, asilimia 5.9 (2019), asilimia 6.1 (2020) na asilimia 5.3 (2021), wakati maambukizi ya homa ya ini aina C yakiendelea kuwa asilimia 2.3 kwa kipindi hicho chote.
Huduma za afya ya akili na lishe pia ilikuwa sehemu ya huduma za wataalamu wa Bugando katika kusherehekea ‘Afya Day’ huku Dk Hijar Kimaro akielimisha kwamba yeyote anayehisi kufikiria vitu visivyo vya kawaida awasiliane na wataalamu kwani hiyo ni dalili ya ugonjwa wa akili. Wazo la kujiua ni dalili pia ya tatizo la akili na msongo wa mawazo uliopitiliza, maarufu kama sonona.
Meneja rasilimali watu wa Kampasi, Alice Mwasyoge, anasema taasisi imehusisha wataalamu wa afya katika sherehe za ‘Afya Day’ ili kuhimiza wananchi kuendelea kujenga utamaduni wa kupima afya zao.
Anasema ni hatua itakayosaidia taifa kuwa na watu wenye afya njema wakati wote kwa maendeleo yao na nchi.
Huduma za ushauri pia ni muhimu, hasa kwa wanafunzi wa kampasi ambao wengi wao wako kwenye umri wa mwanzoni kabisa mwa ujana. Anasema wanafunzi wengi wa kampasi hiyo inayotoa mafunzo ya uchakataji ngozi ni wahitimu wa kidato cha nne, ambao ushauri unapaswa kuwa sehemu ya maisha yao ili waweze kutimiza ndoto zao za kimasomo bila changamoto hasa za kisaikolojia.
“Kwa umri wao huenda wakajiingiza katika mahusiano yasiyo rasmi na kupata mimba zisizotarajiwa pamoja na magonjwa yanayoambukiza ikiwemo VVU hatimaye kushindwa kutimiza malengo yao,” anasema Mwasyoge.
Walio katika mahusiano hayo yasiyo rasmi wanaweza pia kukumbwa na msongo wa mawazo ikitokea kutoelewana baina yao.
“Kwa ujumla hawa ni vijana wadogo ambao bado wanahitaji ushauri wa kitaalamu wakati wote,” anasema.
Mmoja wa wananchi, Isakwisa Jeremiah, anaishauri DIT kuongeza vipimo vingine vya afya katika maadhimisho ya ‘Afya Day’ yajayo, kama vile macho, meno, masikio na VVU. Mbali na huduma za kitabibu, ‘Afya Day’ ilipambwa na michezo mbalimbali iliyoshirikisha vyuo vingine vya mkoani Mwanza kwa mashindano ya mpira wa miguu, pete na mikono, kuruka na kuvuta kamba, kukimbiza kuku pamoja na kukimbia na gunia.
Akizindua tukio hilo, Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela, Said Kitinga, alipongeza juhudi za DIT kushirikisha wataalamu wa afya inashawishi wengi kupima baada ya kusogezewa huduma katika maeneo yao.
Anashauri huduma nyingine kuongezeka katika ‘Afya Day’ ikiwemo uchangiaji damu, akasema hospitali nyingi zinaonesha uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.