Hospitali Arusha kuweka mfumo utunzaji kumbukumbu
HALMASHAURI zote za Mkoa wa Arusha zimetakiwa kufungua mfumo maalum wa ukusanyaji mapato (GoT HoMIS) ambao utasaidia utunzaji wa kumbukumbu ya wagonjwa wanaofika kupata huduma vituoni vya afya.
Agizo hilo limetolewa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella akiwa wilayani Karatu alipotembelea na kukagua hospitali ya wilaya hiyo ikiwemo kuangalia jinsi mfumo wa GoT HoMIS unavyofanya kazi katika udhibiti wa upotevu wa mapato ikiwemo dawa zinazotolewa kwa wagonjwa na zinazoingia vituoni hapo.
Hospitali hiyo iliwekwa jiwe la msingi na Makamu wa Rais ,Dk, Phillip Mpango ambapo serikali imetoa Sh bilioni 3.5 ili kusogeza huduma za afya kwa Wananchi ambao awali walikuwa wakipata huduma za afya wilayani Karatu na Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha.
“Mfumo huu ni vema ukafungwa kwa kila vituo vya afya ili kudhibiti matumizi ya dawa zinazoingia na kutoka ikiwemo kujua takwimu za wagonjwa wanaotibiwa lakini utasaidia ukusanyaji wa mapato”
Pia alisema miradi mingi ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi (Boost )imekamilika vizuri katika mkoa huo na maeneo mengi yameshakamilika na huduma za afya zinaendelea kutolewa ikiwemo vifaa vya kisasa katika hospitali zote za wilaya,hospitali ya mkoa ikiwemo vituo vya afya.
“Kazi ni kubwa inayofanywa na awamu ya sita kupitia kwa Rais Samia Hassan Suluhu na nawaomba wanaarusha tushikmane na tufanye kazi, nawaomba watoa huduma wote wa afya watoe huduma kizalendo na kufuata weledi
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo,Juma Hokororo amesema mradi huo wa afya umefikia asilimia 95 na hospitali hiyo inavifaa vyote vya kisasa na sehemu nyingi huduma za afya zimeshaanza na hivi sasa jengo la upasuaji la wanaume linaendelea kumalizika ujenzi wake.