RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Hospitali ya Wilaya ya Handeni itakuwa maalumu kwa ajili ya tiba ya mifupa.
Alisema hayo alipozungumza na wananchi wa Mkata wilayani ya Handeni katika Mkoa wa Tanga katika siku yake ya kwanza ya ziara mkoani humo jana.
Rais Samia alisema baada ya kutembelea na kuzindua hospitali hiyo aliona kuna wodi mbili moja ikiwa ya jumla na nyingine ya mifupa.
Alisema ni vyema wodi ya mifupa ibaki yenyewe. Amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa apeleke Sh milioni 240 kwa ajili ya kujenga eneo la mifupa katika hospitali hiyo.
“Kwa hiyo wengine wenye kuhitaji huduma za mifupa maeneo mengine watakuja Handeni kwa sababu hatuwezi kusambaza ule utaalamu kwenye hospitali zote kwa hiyo Handeni itabaki kama hospitali maalumu ya mifupa,” alisema Rais Samia.
Mchengerwa alisema serikali ilitoa zaidi ya Sh bilioni 4.37 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
Alisema kutokana na uhusiano mzuri na nchi nyingi ambao Rais Samia ameyatengeneza, wananchi wa Handeni walipata wadau wa maendeleo waliosaidia kujenga majengo na kuifanya kuwa hospitali bora.
Mchengerwa alisema hospitali hiyo inahudumia kata 21, vijiji 91 na vitongoji 770 na imesaidia kuokoa maisha ya watu wengi.
Awashukuru wananchi
Rais Samia aliwashukuru wanakijiji na viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mkata Mashariki kwa kutoa eneo la ekari 32 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
“Ujenzi wa hospitali hii pengine serikali ingenunua eneo kwa fedha zake, mradi ungeweza kuchelewa, walivyotoa eneo mradi umekamilika haraka na wameanza kupata huduma,” alisema Rais Samia.
Alisema hospitali hiyo licha ya kuwa ni ya wilaya, ina viwango vya hospitali ya mkoa kutokana na uwekezaji uliofanyika katika miundombinu na huduma zinazotolewa.
“Wakati natembelea pale nimejuzwa kwamba hospitali ile mpaka sasa imeshapokea wajawazito 900 na 300 kati yao walijifungua kwa operesheni. Usingekuwa ubora wa hospitali hao 300 wangelazimika kwenda hospitali nyingine na kati ya hao si wote wangefika hospitali,” alisema Rais Samia.
Alisema watoto wote walizaliwa salama katika hospitali hiyo isipokuwa wawili waliopoteza maisha baada ya kuzaliwa.
“Kwa mkoa mzima tumejenga hospitali za wilaya tatu, vituo vya afya 15 na zahanati 74, tumeleta magari ya wagonjwa 12, tumenunua mashine mbalimbali za kisasa na tumeongeza watumishi wa afya wa halmashauri karibia 900 na sasa rufaa kwenda nje ya mkoa zimepungua,” alisema Rais Samia.
Alisema katika uongozi wake serikali imetoa Sh trilioni 3.1 kwa Mkoa wa Tanga kwa ajili ya shughuli za maendeleo na amekwenda katika mkoa huo kukagua kazi zilizifanywa kwa kutumia fedha hizo.
Aliahidi kuwa serikali itaendelea kufanya jitihada kupeleka maendeleo nchini kote na kisha wananchi wenyewe waseme kuhusu maendeleo hayo.
Uchaguzi Mkuu
Rais Samia amewakumbusha wananchi wenye sifa za kupiga kura wajiandikishe na kurekebisha taarifa zao ili wapige kura kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Handeni wamduwaza
Aliwashukuru wananchi wa Wilaya ya Handeni kwa mapokezi mazuri na kujitokeza kwa wingi kumsikiliza.
“Wakati naingia eneo hili, kote wamenipokea nikawa najiuliza mbona watu wako njiani. Nilivyoingia hapa nimepigwa na butwaa ndugu zangu, niwashukuru sana sana huu ni upendo mkubwa sana asanteni,” alisema Rais Samia.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema mkutano wa jana Mkata umevunja rekodi ya mikutano mingine aliyowahi kuihudhuria katika eneo hilo.
“Nilikuja mwaka 2005 na 2010 mkutano huu unevunja rekodi. Falsafa ya maandalizi ya umma inasema umma hauandaliwi, umma unakubali wenyewe, Wanatanga wamekukubali wewe,” alisema Makalla.