Hospitali ya Chato yapokea wagonjwa Rwanda, Burundi

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) imeweka wazi kuwa tayari imeanza kupokea wagonjwa kutoka nchi jirani hususani Rwanda, Burundi na Congo (DRC) wanaofuata huduma za matibabu ya kibingwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali Rufaa ya Kanda Chato, Dk Oswald Lyapa amesema hayo mbele ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa msaada.

Viongozi wa Chama na Serikali waliambatana na familia ya Hayati Dk John Magufuli kutembelea na kutoa msaada hospitalini hapo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Miaka minne ya kifo cha Rais huyo wa awamu ya tano.

Dk Oswald amesema, hayo ni matokeo ya upatikanaji wa huduma zote za kibingwa kutokana na uwepo wa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo MRI, CT Scan, kipimo cha magonjwa ya moyo na Mashine 10 za Kusafisha figo.

Amesema hospitali kwa siku inahudumia takribani wagonjwa 105 mpaka 130 na kati yao wanaolazwa ni takribani wagonjwa 10 mpaka 25 kwa siku na pia hospitali inapokea wagonjwa wa rufaa kuanzia 10 na kuendelea kwa siku.

“Wagonjwa ambao tunawapokea kutoka nchi za jirani kwa mwezi ni wastani wa wagonjwa 20 ambao wanatoka nchi za Burundi, Rwanda na Congo (DRC), wanaoongoza sana ni kutoka nchi ya Burundi.

“Wagonjwa hawa wengi wanaokuja hasa wanakuwa na magonjwa ya moyo, magonjwa ya mifupa, lakini wengine ni upasuaji hasa hasa tezi dume pamoja na magonjwa ya ugumba”, amesema Dk Oswald.

Amesema utoaji wa huduma kwa raia wa kigeni si tu inaongeza mapato kwa hospitali bali pia inachangia maendeleo ya kiuchumi kwa wafanyabiashara kwani wanapokuja wanapata huduma za malazi wilayani Chato.

Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk Medard Kalemani amesema mpaka kukamilika hospitali hiyo inatarajiwa kugharimu sh bilioni 38.75 kati ya hizo sh bilioni 18 zilitolewa na kutumika chini ya serikali ya awamu ya tano.

“Mama Samia alikuja kukamilisha na mpaka sasa mradi unatumika, yeye ndio aliyeongeza bilioni 14 nyingine na kufikia shilingi bilioni 32.7 na tulimuomba na tayari ameongeza bilioni sita zingine”, amesema.

Binti wa Hayati Dk Magufuli, Jesca Magufuli amesema familia inafarijika kuona miradi ya kimkakati ambayo iliachwa na baba yao inaendelea kutekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Rehema Sombi amewaomba watumishi na wananchi wote kulinda miundombinu ya hospitali hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button