White: Miedema ataifunga Arsenal
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Uingereza, Ellen White amesema anahisi imeandikwa mbinguni kwamba nyota Vivianne Miedema ataifungia Manchester City watakapokutana na timu yake ya zamani Arsenal katika mechi yao ya ufunguzi ya Ligi ya Wanawake msimu wa 2024-25.
Miedema, 28, alifunga mabao 125 katika mechi 172 katika michuano yote kwa kipindi cha misimu saba akiwa ‘The Gunners’.
Hata hivyo, Arsenal walifanya uamuzi wa kutomuongezea mkataba Miedema, huku City wakimsajili msimu wa joto baada ya kuwa mchezaji huru.
SOMA: Man City yaingia kwenye rada za Arsenal
Muholanzi huyo atarejea uwanja wa Emirates siku ya Jumapili huku Arsenal wakiwakaribisha City katika kile kinachoaminiwa kuwa wikiendi ya kusisimua ya ufunguzi wa WSL.
“Itakuwa tofauti kwake, itakuwa ajabu kidogo, lakini anaonekana kuwa na furaha na hilo ndilo jambo kubwa kwa Viv,” amesema White kwenye kipindi cha Wiki cha Soka cha Wanawake cha BBC Radio 5 Live.