ICTC yatembelea kiwanda bidhaa za Tehama

KATIKA kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa imefanyika jijini Arusha jana, Mkuu wa Utawala na Rasilimali Watu wa Tume ya Tehama nchini (ICTC), Flora Salakana aliongoza timu ya wanawake 10 kutembelea kiwanda cha cha wazawa cha TanzTech Electronics Limited kinachounganisha bidhaa za Tehama.
Moja ya sababu iliyowasukuma wanawake hao kutoka ICTC kutembelea kiwanda hicho ni ukweli kwamba asilimia 90 ya watu walioajiriwa kiwandani hapo ni wanawake.
Akizungumza baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Salakana alisema wanajisikia fahari kuwa na kiwanda hicho cha kuunganisha vifaa vya Tehama nchini na kutoa kipaumbele kikubwa cha ajira kwa wanawake.
Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuvutia uwekezaji wa ndani na kuzingatia suala la usawa wa kijinsia nchini.

Wafanyakazi wa Tume ya Tehama nchini (ICTC) wakiwa kwenye picha ya pamoja walipotembelea Kiwanda cha TanzTech Electronics jijini Arusha mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto walioketi ni Mkuu wa Utawala na Rasilimali Watu wa Tume hiyo, Flora Salakana, aliyeketi katikati mbele ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha TanzTech, Gurveer Hans (Picha na ICTC)
“Kwa kweli tumekuja kutembelea kiwanda hiki kama sehemu yetu ya kujifunza namna kiwanda hiki kinavyofanya kazi ya kuunganisha vifaa vya Tehama. Jambo la kuvutia zaidi ni kwamba asilimia 90 ya wafanyakazi mliowaajiri hapa ni wanawake na ukizingatia kesho (leo) ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani,”alisema Salakana.
Aliongeza”Tunawapongeza kwa kuwajengea vijana wa kike ujuzi kwa kuwapatia mafunzo ya miezi ya miezi mitatu ya namna ya kuunganisha vifaa vya Tehama. Sisi kama Tume ya Tehama pamoja na Wizara yetu ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tupo tayari kuwaunga mkono kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Gurveer Hans aliwaeleleza akina mama hao wataalamu wa masuala ya Tehama kutoka Tume ya Tehama kuwa walipotangaza nafasi za kazi walijitokeza watu zaidi ya 120 na waliopasi usaili walikuwa 60 na asilimia 90 ya 60 waliowaajili ni wasichana waliohitimu kidatu cha nne.
Alisema waliwapatia mafunzo ya miezi 3 kabla ya kuwaajiri na wanafanya kazi vizuri ya kuunganisha vifaa vya Tehama ambavyo ni vya kisasa.
Hans alivitaja baadhi ya vifaa hivyo wanavyoviunganisha kiwandani hapo kuwa ni pamoja na simu janja, mita za kisasa za maji za malipo kabla ya huduma, projekta ambayo ina matumizi mengi kwa ajili ya kufundishia wanafunzi, kompyuta mpakato na bidhaa nyingine nyingi.
Pia alisema baada ya kipindi cha kama miezi mitatu ijayo wanatarajia kuzifikisha bidhaa zao sokoni na watafungua maduka katika kila mkoa ili wananchi wengi wamudu kuzipata bidhaa zao kwa gharama nafuu.



