IJP, wenzake waomba zuio uchunguzi kifo cha utata

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imeshindwa kuanza utekelezaji wa amri iliyotoa Februari 17, mwaka huu ya kufanyika uchunguzi wa chanzo cha kifo cha mfanyabiashara, Stella Moses anayedaiwa kupoteza maisha akiwa mahabusu ya kituo cha Polisi Mburahati mwaka 2020.

Mahakama imeshindwa kutekeleza amri hiyo baada ya upande wa wajibu maombi ambao ni Mkuu wa Jeshi la Polisi na wenzake kuwasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2022.

IJP na wenzake wameomba uchunguzi huo usifanyike mpaka maombi waliyoyawasilisha yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Wakili wa mleta maombi, Peter Madeleka alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya utekelezaji wa amri ya kufanyika kwa uchunguzi wa kifo cha Stella ambaye alikufa katika mazingira ya kutatanisha.

Alidai kuwa akidi imetimia kwa maana ya kuwepo kwa wazee watatu wa baraza kwa ajili ya kushuhudia ufukuaji wa mwili na kufanyika kwa uchunguzi huo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema alipinga hoja hiyo akidai kwamba Februari 17 mwaka huu walifungua shauri la uchunguzi namba moja la mwaka 2023 wakitaka uchunguzi wa kesi hiyo ufanyike.

Mrema alidai kuwa wanafahamu kwamba mahakama ilitoa amri kuhusu kufanyika kwa uchunguzi lakini wanaomba kusikilizwa kwa shauri lao kwanza.

Wakili Madeleka alipinga hoja ya Mrema akidai kuwa linalenga kuipotezea muda mahakama na kwamba upande wa serikali haukutaja kifungu cha sheria ambacho kimekiukwa kwa kuwepo kwa shauri hilo mahakamani.

Alidai kuwa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya James Rugemalira dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) iliamuru kwamba ili pingamizi likubaliwe linatakiwa kutaja kifungu cha sheria iliyovunjwa.

Alidai kuwa Ibara 107 A na B ya Katiba imebainisha kuwa mahakama ni chombo huru na kwamba katika kutekeleza majukumu yake katika mashauri ya jinai na madai italazimika kuzingatia masharti ya katiba na ya sheria za nchi.

“Mpaka leo tuko hapa maana yake kesi ipo mbele yako mheshimiwa na umeisikiliza na kutoa amri hivyo kilichobaki ni utekelezaji wa amri ili kujua sababu za kifo…mahakama haijawahi kufanya uchunguzi na sababu hazijajulikana,” alidai Madeleka.

Aliendelea kudai kuwa endapo mahakama ingekuwa imefanya uchunguzi na sababu zikajulikana, maombi hayo ndio yangeletwa mahakamani kwa kuwa mpaka sasa kesi hiyo haijafika kikomo.

Alidai maombi yaliyowasilishwa mahakamani yameletwa kinyume na sheria kifungu cha 4, 12 cha Sheria ya Uchunguzi wa Kifo na kwamba kama shauri hilo lipo linakiuka katiba.

Wakili Mrema alidai sheria haiwazuii kuleta pingamizi na kwamba wana uwezo wa kuwasilisha pingamizi hata kama kesi inakaribia kutolewa hukumu.

“Kwa kuwa uchunguzi haujafanyika tunasisitiza kilichoombwa ni amri ya kufanya uchunguzi na kwa mujibu wa maombi yetu ipokee kama mambo ya kufikirika ambayo yamewasilishwa,” alidai.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 17 mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi dhidi ya mapingamizi hayo.

Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020 akiwa mahabusu ya kituo cha Polisi Mburahati alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa anahitajika. Polisi walidai kuwa Stella alijinyonga.

Wanafamilia waliomba ufanyike uchunguzi huru na shauri hilo lilifunguliwa na shemeji wa marehemu, Emmanuel Kagongo kwa niaba ya familia ya marehemu.

Alifungua shauri hilo dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspekta Jenerali wa Polisi – IJP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button