Imani, mila zatajwa vifo vya wanawake, watoto

IMANI, mila na desturi za kitamaduni, ukosefu wa usawa wa kijinsia ni miongoni mwa sababu zinazorudisha nyuma udhibiti wa magonjwa na vifo vya akina mama na watoto wachanga nchini.

Hayo yameelezwa, jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Angellah Kairuki katika makabidhiano ya majengo, vifaa vya huduma za dharura za afya ya uzazi ya mama na mtoto na gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha Dabalo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, msaada uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA) kupitia mradi wa RMNCH unaotekelezwa na TAMISEMI.

Waziri Kairuki amesema kuwa kuna mambo makubwa mawili yanayokwamisha juhudi hizo za kupunguza vifo na kusema kuwa ni yale yanayohusu mfumo wa afya na yaliyo nje ya mfumo wa afya.

“Kuna sababu zinazorudisha nyuma udhibiti wa magonjwa na vifo vya akina mama na watoto wachanga nchini, miongoni mwa hizo ni mambo yanayohusu mfumo wa afya, ikiwa ni pamoja na kutotekelezwa ipasavyo kwa sera, miundombinu dhaifu ya afya, upatikanaji mdogo wa huduma bora za afya.

“Uhaba wa rasilimali watu, upungufu wa wahudumu wa afya wenye ujuzi, mifumo dhaifu ya rufaa, ukosefu wa vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi na uratibu duni kati ya sekta za umma na sekta binafsi.

“Sababu nyingine ni mambo yaliyo nje ya mfumo wa afya ikiwa ni pamoja na ushiriki duni wa jamii na ushirikishwaji katika kupanga, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya wa huduma za afya, baadhi ya imani, mila, na desturi za kitamaduni, ukosefu wa usawa wa kijinsia, na kutokuwa na tabia za kutafuta huduma za afya kwa wakati, pindi changamoto za kiafya zinapoanza kujitokeza.

“Ili kukabiliana na changamoto hizi kunahitajika juhudi za pamoja kati ya serikali na wadau wengine wa maendeleo katika sekta ya afya pamoja na sekta nyingke Mtambuka.

“Makabidhiano tunayoshuhudia leo ni sehemu ya juhudi hizi za pamoja kati ya UNFPA, Serikali ya Denmark na Serikali ya Tanzania,” amesema Kairuki.

 

Kairuki amesema kuwa anatambua mchango wa UNFPA, Serikali ya Denmark na Serikali ya Tanzania kupitia OR-TAMISEMI, Mkoa wa Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino katika kuboresha Zahanati ya Dabalo kuwa kituo cha afya, ili kiweze kutoa huduma za dharura na upasuaji kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga, kuimarisha mifumo ya rufaa kwa kutoa gari la kubebea wagonjwa, lakini pia kutoa vifaa muhimu vya matibabu kwa kituo cha afya cha Dabalo, na Zahanati  nyengine tatu zaidi  za Manda, Itiso  na Nhinhi.

“Kupitia msaada huu, Zahanati ya Dabalo imeboreshwa na kuwa Kituo cha afya (ukarabati/ujenzi, vifaa) ili kuweza kutoa huduma za dharura na upasuaji kwa wajawazito na watoto wachanga.

“Zahanati tatu (Manda, Itiso na  Nhinhi) zimepatiwa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kutoa huduma za Msingi kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga na gari moja la kubebea wagonjwa limenunuliwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za rufaa kwenye Wilaya hii. Aidha, kituo  cha huduma rafiki kwa vijana kimejengwa na kuanza kutoa huduma katika zahanati ya Nhinhi,” amesema Waziri Kairuki.

Ameongeza kuwa gharama za msaada huo ni  jumla ya Sh 615,205,539, ambapo Sh 327,000,000 zimetumika kwa ukarabati na ujenzi na Sh 288,205,539 zimetumika kwa ununuzi wa gari la kubebea wagonjwa na vifaa na vifaa tiba.

Awali mwakilishi wa UNFPA nchini Tanzania, Mark Bryan Schreiner alisema kuwa wanatambua dhamira ya pamoja na Serikali ya Tanzania kutoa haki na chaguo kwa wote, na kwamba wanaheshimu kujitolea kwa wahudumu wa afya katika kutoa huduma za afya ya uzazi na jinsia.

“Tunaitambua serikali ya Denmark kama mtetezi thabiti wa kimataifa wa afya ya uzazi na haki za uzazi, na Ubalozi wa Kifalme wa Denmark jijini Dar es Salaam kwa kusaidia uimarishaji wa mfumo wa afya, ili kupanua uwezo wa huduma za afya ya uzazi nchini Tanzania,” alisema.

Balozi wa Denmark nchini, Mette Norgaard amesema: “Kupitia utoaji wa huduma za afya ya uzazi na taarifa, mradi unaofadhiliwa na Denmark umeleta mabadiliko katika maisha ya makumi ya maelfu ya wanawake, wanaume na vijana,” amesema

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x