SERIKALI ya India inatarajia kuanzisha Chuo cha Teknolojia nchini Tanzania, ambacho kitakuwa kinatoa kozi ya masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), pamoja na kozi nyingine zinazoendana na mlengo huo.
–
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema hayo jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na Balozi wa India nchini, Binaya Pradhan pamoja na timu ya wataalam kutoka chuo hicho.
–
Amesema serikali ya Tanzania itashirikiana na nchi ya India, ili lengo la kuanzisha chuo hicho liweze kutimia kwa wakati, ili wanafunzi wasajiliwe mwaka mpya wa masomo ifikapo Novemba mwaka huu.
–
Amesema Chuo hicho cha Teknolojia kipo mbali kiteknolojia ndio maana wamekialika kuja kuona mazingira ya Tanzania katika kutimiza lengo lao la kuanzisha chuo hapa nchini.
–
“Wenzetu hawa wanataka kuanzisha chuo hapa nchini tuliwaalika waje na tayari wamefanya mazungumzo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuahidiwa ardhi kwa ajili ya kuanzisha huko, lakini kwa kuwa suala la elimu ya juu ni la Muungano tunaangalia taratibu kuona nini kinaweza kufanyika, ili kazi hii iweze kuanza.
“Wanataka kuanza kuchukua wanafunzi Oktoba mwaka huu ni muda mfupi sana kutokea sasa, ila tutafanya kazi usiku na mchana kuona ni nini kinaweza kufanyika tukasonga mbele,” amesema.
Mbali na kufikia Dar es Salaam timu hiyo kutoka India imekwenda kutembelea Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela kilichoko jijini Arusha pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ili kuona vifaa vya kujifunzia na kufundishia vilivyopo na namna ambavyo wanaweza kufanya kazi kwa pamoja.
“Timu hii tutakutana nayo tena Februari 17 mwaka huu ili kwa pamoja tuangalie rasimu ya makuballiano ili tuone tunakwendaje,” amesema .
Kwa upande wake Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Pradhan amesema Serikali ya India imejizatiti kufanya kazi na Serikali ya Tanzania, ili kuhakikisha pamoja na mambo mengine lengo la kuanzisha chuo nchini Tanzania linafanikiwa.