DAR ES SALAAM – TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema haiwezi kusimamia na kuratibu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu kwa kuwa sheria haijaipa mamlaka na itakapopewa mamlaka haitakuwa na muhali kutekeleza jukumu hilo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima alisisitiza wananchi kuachana na kile alichosema ni upotoshaji unaoendelea kuhusu mamlaka inayopaswa kusimamia uchaguzi huo.
Alitoa ufafanuzi huo katika mkutano wa INEC na wanahabari kujadili kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na mfumo wa kidijiti wa maboresho.
Hivi karibuni Chama cha ACT Wazalendo kilipinga Tamisemi kuendelea na mchakato wa maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kikisema ni batili, ukiukwaji wa sheria na kwamba kuendelea kufanyika kutatia doa serikali.
Kilisema kuwa hata wajumbe na viongozi wa tume waliopo ni batili kwa kuwa walipaswa kujiuzulu ili kupata viongozi wapya kwa utaratibu ulioainishwa kwenye sheria mpya.
Kailima alisema jukumu la uchaguzi wa serikali za mitaa litaendelea kubaki mikononi mwa Tamisemi hadi itakapotungwa sheria.
Alisema ikishatungwa, tume haitakuwa na muhali kuitekeleza. Alisema upotoshaji mwingine ni unaodai kwamba kuna sheria mbili zilizokuwepo ambazo zimefutwa.
Ikidaiwa ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge namba 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Madiwani namba 292.
SOMA: Wanaotafuta ajira serikalini waongezeka – Ripoti
Kwa mujibu wa Kailima, upotoshaji huo unadai kwamba Tamisemi haipaswi kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa sheria hizo zimefutwa.
Alifafanua zaidi, “kuna mtu anapotosha anasema sheria hizi zimefutwa, anashindwa kufahamu kwamba zipo sheria tofauti nyingine namba 288 na 287 ambazo zinaweza kutumika.”
Kuhusu uhalali wa tume inayoendelea kufanya kazi na wajumbe wake, alisema inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri, akithibitisha kupitia kifungu cha 27 cha Sheria Mpya ya INEC.
“Twende kwenye sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu cha 27 kinasema mara baada ya kuanza kutumika kwa sheria hii mtu yeyote ambaye ni Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti au Mjumbe wa tume, ataendelea kushika madaraka hayo hadi pale muda wake utakapokuwa umekoma,” alisema.