Iran yasifu fursa za uwekezaji Tanzania

SERIKALI imewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mazingira salama ya biashara na uwekezaji.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk alibainisha  hayo alipofungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Iran lililofanyika Jumatano Dar es Salaam.

Balozi Mbarouk alisema Tanzania imejitahidi kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwavutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi waje kuwekeza nchini.

“Tunapoendelea na juhudi za kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza uwekezaji nchini Tanzania, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Iran kuwekeza nchini Tanzania kwani ni nchi yenye amani, utulivu na iliyojaliwa kuwa na maliasili nyingi hasa katika maeneo ya kimkakati yakiwemo mafuta na gesi, madini, viwanda, utalii, uchumi wa bluu, kilimo na mifugo,” alisema Balozi Mbarouk.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Amir Abdollahian alisema kongamano hilo la biashara na uwekezaji litatoa fursa kwa  wafanyabiashara alioambatana nao na  kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana Tanzania.

Abdollahian alikiri kuwa Tanzania ina fursa nyingi zinazohamasisha na kuvutia biashara na uwekezaji. “Tumeridhishwa na juhudi za serikali ya Tanzania za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na tunaahidi kuwa tutaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kutoka Iran kuja kuwekeza Tanzania,” alisema Abdollahian.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button