- Kwa sasa anamiliki kiwanda, biashara 18
- Ana tuzo tatu, ikiwemo ya Malkia wa Nguvu
MITANDAO ya kijamii imekuwa changamoto kwa baadhi ya watu, lakini imekuwa msaada mkubwa na mwanzo wa maisha ya mafanikio kwa wengine.
Kufanikiwa kwako au kuanguka kwako inategemea njia gani umekuwa ukiitumia, ambayo kwako unahisi sahihi.
Mfanyabiashara Irnestina Mwenda ‘Coconut Lady’ anaeleza mitandao ilivyomtoa kuwa mama wa nyumbani mlezi wa mtoto hadi kuwa mjasiriamali aliyetunukiwa tuzo.
Mwanamama huyo anasema baada ya kuachana na kazi katika kiwanda cha kinywaji ili kulea mtoto, alikumbana na changamoto ya kutotoa maziwa ya kutosha na mtoto kupata mafua mara kwa mara kutokana na mafuta ya nazi aliyokuwa akiyatumia.
Anasema kuitia mitandao ya kijamii alifanikiwa upata suluhisho kwa changamoto hiyo, lakini pia alifungua kampuni ya kibiashara ya Mama Active na kuwa miongoni mwa wajasiriamali wachache wanaosaidia wakulima kwa kuchukua bidhaa kutoka shambani moja kwa moja.
Anaelezea safari yake ya mafanikio ilivyoanza kuwa Februari, mwaka 2016 alianza biashara yake rasmi, wakati alipokuwa akitafuta suluhisho la kutafuta maziwa ya kumnyonyesha mtoto wake wa kwanza.
Anasema mwaka 2015 alifanikiwa kupata mtoto wa kwanza, lakini alikuja na changamoto ya kutotoa maziwa ya kutosha kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto wake huyo.
Changamoto hiyo ilimfanya mumewe kumuachisha kazi kwenye kiwanda cha soda, ambapo alikuwa akihudumia kama Ofisa Uzalishaji akarudi nyumbani ili kupata nafasi ya kumnyonyesha mtoto wake.
Irnestina anasema baada ya kuona changamoto imekuwa kubwa akafungua akaunti ya mtandao wa kijamii wa Instagram na kuanza kuuliza watu jinsi gani anaweza kutengeneza maziwa ya kutosha kwa mtoto wake.
Kupitia mitandao ya kijamii alijifunza namna ya kupata maziwa ya kutosha, kupitia mbegu za maboga ambazo zina madini chuma kwa wingi, protini na madini mengine ambayo yanasaidia kuzalisha maziwa na kumsaidia mtoto.
“Nikajikuta mimi nakuwa mtoa huduma mkubwa katika ukurasa wangu kuhusiana na changamoto za mama na mtoto. Watu wengi wakawa wananipenda na kunifuatilia kupitia mtandao wangu,” anasema.
Kutokana na mafanikio hayo, anasema alianza kutengeneza unga wa mbegu za maboga kwa ajili ya matumizi yake mwenyewe, lakini wenzake wakaanza kumsifia na kutaka wauziwe.
“Watu walianza kuniunga mkono na baadhi ya rafiki zangu kwenye mitandao ya kijamii, walianza kuniomba niwatengenezee na kuwauzia.
Hivyo nikaanza na mifuko mitatu, na kuwauzia wakawa wanatangaziana nikajikuta nikipigiwa simu na watu wengine ambao sikuwawajua,” anaeleza.
Anasema wakati akiendelea na biashara ya kuuza unga wa mbegu za maboga, kulikuwa na changamoto nyingine kwa mwanaye, ya kupiga chafya mara kwa mara na kupata mafua kutokana na kutumia mafuta ya kiwandani.
Changamoto hiyo alipokuwa akiandika katika makala zake za mtandaoni, aligundua sio tatizo la mtoto wake peke yake ila linawasumbua wengi, hivyo akahakikisha anatafuta suluhisho.
Anasema katika kutafuta suluhisho la ngozi ya mwanaye na kuepukana na chafya na mafua, alitengeneza mafuta ya nazi ambayo hayapitii kiwandani , kwa kupata elimu zaidi kupitia semina zinazotolewa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO).
Elimu ambayo aliipata SID, ilimuwezesha kubadili mfumo wake wa uzalishaji kutoka nyumbani hadi kuwa na kiwanda kidogo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.
Anasema alianza kutanua biashara zake kutoka biashara moja ya unga wa maboga hadi kufikia biashara 18 na wafanyakazi 17 katika kiwanda chake kidogo kilichokuwa Kawe jijini Dar es Salaam lakini pia amezalisha ajira zingine kupitia bidhaa zake huko mtaani.
Lakini pia akaacha kuchukua mzigo Kariakoo na kwenda mashambani moja kwa moja kununua mazao kutoka kwa mkulima kwakuwa alikuwa akihitaji malighafi nyingi zaidi.
Alianza kutengeneza biashara nyingine kama mafuta ya nazi Virgin Active Mama, Unga wa begu za Maboga, Sabuni za watoto, sabuni za wakubwa, siagi za karanga, shampoo, unga wa uji na vitu vingine kwa kupitia kampuni yake ya Active Mama.
Anasema alianza kusafiri mikoani kufuata mali ghafi kama vile nazi anazozifuata Mafia, Kilwa, Lindi, karanga mkoani Tanga, mbegu za maboga mkoani Iringa, Mbeya na Tanga naa kuanzisha mashamba ya mahindi.
“Nanunua malighafi hadi kwa tani, hivyo nasaidia wakulima katika shughuli zao za kilimo kwa kuwa tayari wengine walikuwa na uhakika wa mazao yao kununuliwa,” anaeleza Irnestina.
Anasema ilipofika mwaka 2020, alimtafuta mtu wa kusimamia kazi zake ili asibweteke na kujiona kwamba tayari ameshafanikiwa na kumpata John Ulanga.
Anaeleza kuwa alizungumza na Ulanga na kwa pamoja wakaweka mkakati wa namna ambavyo anaweza kufanya kazi na kupeleka matokeo ya biashara ili kuweza kumnoa na kumtengenezea mwongozo ingawa alipitia changamoto nyingi.
Irnestina anasema alianza kupata tuzo akiwa kama mjasiriamali aliyefanikiwa katika biashara yake na kupata tuzo ya Malkia wa Nguvu 2018 iliyoandaliwa na Clouds FM, Woman Of The Years 2021 iliyoandaliwa na Dina Marious na Best Loca Brand on Digitat 2021 iliyoandaliwa na Tanzania Digita.
Anasema baada ya hao akawa mwalikwa katika semina za kijasiriamali na akawa mtoa mada katika shughuli mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kujikwamua katika dimbwi la umaskini.
Mafanikio mengine aliyopata anasema kwa sasa bidhaa zake zinafika karibu Tanzania nzima lakini sehemu ambazo soko lake lipo kwa wingi ni Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Moshi, Mwanza na Nairobi.
Mwanamama huyo anaeleza matarajio yake katika miaka mitatu ijayo kuwa ni kusambaza bidhaa zake katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili uleta ushindani na kampuni nyingine za nje.
Kuhusu changamoto anasema amekutana na za kawaida katika biashara, lakini miongoni mwa changamoto kubwa ni kuingiza bidhaa mpya wakati watu kuna bidhaa tayari wamezizoea.
“Nilikuwa natupiwa bidhaa zangu, lakini sikukata tamaa. Kila mtu anakuwa anaamini ile bidhaa nyingine ni sahihi kwake,” anasema.
Changamoto nyingine anasema ni katika soko, bado kuna kazi kubwa kulikamata soko la nchi nzima hususani katika kuwaaminisha wateja kuhusu ubora wa bidhaa husika.
Akizungumzia historia yake, Irnestina anasema kwa sasa yeye ni mama wa watoto watatu, na anaishi na mumewe, amezaliwa wilaya ya Shinyanga Mjini mkoani Shinyanga na kusomea elimu yake ya msingi katika shule ya Kambarage na kumaliza mwaka 2000.
Anasema alijiunga na elimu ya Sekondari katika shule iliyopo wilayani Tarime, akajiunga na kidato cha tano na sita Msalato ambapo alichukua mchepuo wa PCB (Physics, Chemistry na Mathematics).
Anasema baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika fani ya Uhandisi wa Viwanda na baada ya kumaliza aliajiriwa kwenye kampuni ya vinywaji kama Ofisa Uzalishaji.