VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuisemea kwa nguvu Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, ili kushawishi uharakishwaji Kwa watoa maamuzi ili ifanyiwe marekebisho.
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu wasichana kuolewa wakiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya mahakama na kuanzia umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi.
Hata hivyo, sheria hiyo imekua ikipingwa na wanaharakati mara kadhaa, na mahakama nchini iliamuru kubadilishwa na umri wa kuolewa kwa watoto wa kike uanzie miaka 18 na kuendelea.
Lakini tangu kutolewa kwa uamuzi wa mahakama miaka zaidi ya mitatu imepita bila mabadiliko hayo kutekelezwa.
Matatizo yaliyopo katika sheria hiyo ni pamoja na kukianzana na sheria ya mtoto, ambayo inamtafsiri mtoto kama mtu yoyote aliyeko chini ya umri wa miaka 18.
Hata hivyo hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa wanashughulikia mabadiliko ya sheria hiyo kandamizi kwa mtoto wa kike.
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo kwa Waandishi Mahiri wa Habari za Watoto, Naibu Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Ousmane Niana, amesema pamoja na vyombo vya habari kufanya kazi kubwa ya mapambano ya kuandika habari za ukatili kwa watoto na kupunguza hali ya utapiamlo nchini, bado vina jukumu kubwa la kuelekeza nguvu katika kuisemea kwa nguvu zote sheria ya ndoa kwa mtoto iweze kufanyiwa mabadiliko.
“Kila Mtanzania ana jukumu la kuhamasisha kuzuia watoto kuolewa wakiwa na umri mdogo, ili waweze kusoma na kufikia ndoto zao,” anasema Niana na kuongeza:
“Tunahitaji vyombo vya habari ili kukuza kampeni katika chaneli zetu zote, ili watu zaidi wafahamu kuihusu na kuchukua hatua inayohitajika, ” amesema.
Kwa mujibu wa takwimu za Unicef za mwaka 2017, katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.
Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya umri wa miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40. Tanzania ni asilimia 31.
Nchini Kenya, ni watoto asilimia 23 wanaoozwa kabla ya kutimiza miaka 18
Ripoti hiyo imeeleza kuwa nguvu kubwa ya kutokomeza tatizo hili la ndoa za utotoni ilihamia Afrika, ambapo jitihada zaidi zilihitajika ili kupunguza tatizo hilo.
Umoja wa Mataifa huchukulia ndoa za watu wa chini ya miaka 18 kuwa ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Niana amesema katika takwimu za sensa zilizotolewa Oktoba mwaka huu, idadi ya watoto Tanzania ni asilimia 50, mwaka 2020 idadi ya watoto nchini ilikua milioni 28 na makadirio yanaonesha kuwa idadi ya watoto Tanzania itaongezeka maradufu na kufikia karibu milioni 59 ifikapo mwaka 2050.
Naye, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema “Tutashiriki kikamilifu kupinga ndoa za utotoni kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanatimiza ndoto na malengo yao.”
Akilishukuru Shirika la Maendeleo la Kusaidia Watoto (UNICEF), Balile amesema kabla ya mradi huo wa habari za watoto kuanza kuendeshwa nchini msamiati wa udumavu haukuwa ukifahamika sana nchini.
Amesema: “Tunawashukuru Wahariri kwa kuwafahamisha wananchi mambo kama haya. Lakini tunawashukuru waandishi wa habari kwa kutumia gharama, muda wetu katika kutafuta habari hizi za watoto, gharama mnazozitumia ni kubwa kuliko kiwango cha zawadi mnazotunukiwa leo. Niwaombe UNICEF ushirikiano huu uliozaa matunda msituache.”
Naye Jesse Kwayu, Mjumbe Kamati ya Mradi wa Habari za Watoto amesema kazi ya kuwa na habari za watoto ni kuwapa kipaumbele waweze kusikika.
Amesema: “Kumekuwa na kazi nzuri zimefanyika habari 76 zimeandikwa na kutangazwa, ni mafanikio makubwa pamoja na mafanikio haya yako mambo ya kuangalia tangu mwaka 2017 na leo tunaingia 2023 kuna impact gani.”
Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kuweka msisitizo katika kuhamasisha umma kutoa maoni yao kupinga sheria inayoruhusu ndoa za utotoni.
“Kutoka hapa tunafanya nini katika sheria ya ndoa, je, waandishi kwa ujumla wetu tunaifahamu hii Sheria ya Ndoa ya 1971?
“Lengo tujikiite kufanya kampeni ili iweze kufanyiwa mabadiliko, lengo mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18 aweze kutimiza malengo na si kuolewa katika umri mdogo ambao ni chini ya miaka 18,” amesema Kwayu.