ISRAEL:WAZIRI wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameahidi kuongeza mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza ikiwa kundi la wanamgambo la Hamas litaendelea kurusha maroketi kuelekea Israel.
Katz amesema kuwa ikiwa Hamas haitaruhusu kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza, basi watakabiliwa na mashambulizi makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu.
Waziri Katz alitoa kauli hiyo alipokuwa akitembelea mji wa Netivot, ulio karibu kilometa 16 Mashariki mwa Palestina. SOMA: Israel kujadili azimio la Beirut
Awali, Jeshi la Israel (IDF) lilichapisha ujumbe kwenye ukurasa wake wa X, likisema kuwa kundi la Hamas lilifyatua roketi mbili katika mji wa Netivot wakati wa mkesha wa mwaka mpya.
Katz aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi mwezi Novemba baada ya mtangulizi wake, Yoav Gallant, kufutwa kazi kufuatia tofauti na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.