Israel yaruhusu malori100 ya misaada kuingia Gaza

GENEVA : UMOJA wa Mataifa umethibitisha kuwa umepata kibali kutoka kwa Serikali ya Israel kuruhusu malori takribani 100 yaliyojaa misaada ya kibinadamu kuingia katika Ukanda wa Gaza.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA), Jens Laerke, amesema kuwa kibali hicho kinatoa nafasi kwa shehena kubwa ya misaada kuwasilishwa kwa wakazi wa Gaza ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.
“Tuliwasilisha ombi la kuingiza malori mengi zaidi ya yale yaliyoidhinishwa awali, na tumepata idhini hiyo. Tunatarajia kwamba ifikapo leo (Jumatano), malori hayo yatachunguzwa na kuruhusiwa kuvuka hadi kufika maeneo ya ndani ya Gaza kwa ajili ya kusambaza misaada,” alisema Laerke.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inaleta matumaini kwa maelfu ya raia wa Palestina waliokwama katika mazingira magumu kutokana na ukosefu wa chakula, maji safi, na dawa muhimu.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, misaada hiyo ni pamoja na vyakula, dawa, na vifaa vya huduma za dharura, ambayo imekuwa ikicheleweshwa kuingia Gaza kutokana na masharti na vizuizi vilivyowekwa na Israel tangu kuanza kwa mvutano unaoendelea.
Misaada hiyo ilianza kuingia Gaza Jumatatu kwa mara ya kwanza tangu zaidi ya miaka miwili, hatua iliyofuatia shinikizo kubwa la kimataifa dhidi ya Israel kuhusiana na kuzuiwa kwa misaada hiyo.
Katika siku za hivi karibuni, Israel imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, wakihimiza kuruhusu misaada kufika kwa raia wanaoteseka kutokana na mzozo unaoendelea.
SOMA: Netanyahu awashutumu viongozi wa Ulaya kuhusu Gaza