JAB yabana waandishi waliotangaza nia ya kugombea

BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewabana waandishi wa habari waliotangaza nia ya kugombea nafasi za kisiasa kwa kuwataka kusitisha mara moja shughuli zote za kihabari katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
Maelekezo hayo yalitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Patrick Kipangula kupitia taarifa kwa umma aliyoitoa jana.
Alisisitiza umuhimu wa waandishi kuzingatia sheria, maadili na kanuni za taaluma ya habari hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Kipangula, hatua hiyo inalenga kuepusha mgongano wa kimaslahi, kulinda uaminifu wa vyombo vya habari na kuhakikisha mazingira ya usawa kwa wagombea wote.
Alifafanua kuwa kuendelea kwa watia nia kufanya kazi za kihabari ni ukiukwaji wa Kanuni ya 12 (g) ya Kanuni ya Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa, iliyotolewa kupitia Tangazo la Serikali Na 775 la Septemba 2020.
Aidha, bodi hiyo imeelekeza kuwa waandishi wote wanaofanya kazi katika vyombo vya habari bila kujisajili kupitia Jab wanapaswa kuacha mara moja hadi watakapokamilisha mchakato wa usajili wao kupitia mfumo wa Tai Habari.
Kipangula alisema kuendelea kufanya kazi pasipo usajili ni uvunjifu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, ambayo inakataza mtu yeyote kufanya kazi za kihabari bila ya kupata ithibati kutoka kwa Bodi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Bodi ya Ithibati itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa waandishi wa habari nchini na haitasita kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuwataja hadharani wale watakaobainika kukiuka masharti ya sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Mwisho