Jafo aagiza udhibiti mipakani mifuko ya plastiki

IKIWA leo inaanza opereshani ya nchi nzima ya kutokomeza matumizi ya mifuko ya plasiki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo ametaka kuongeza udhibiti katika mipaka ili kuzia uingizaji mifuko hiyo.

Akizungumza jijini hapa, Dk Jafo alisema serikali imekuwa ikikamata shehena za mifuko ya plasitiki kutoka nje zikiwemo tani tisa zilizokamatwa hivi karibuni jijini Mwanza.

“Nadhani baadhi ya nchi majirani bado wanatumia mifuko ya plastiki, maana tumekuwa tukikamata shehena za mifuko hiyo maeneo na kanda mbalimbali ambapo mizigo mingine imekuwa ikitoka nje ya nchi ikipita katika mipaka yetu jambo hili haliridhishi hata kidogo.”

Dk Jafo alisema kuwa Tanzania imejiwekea sheria na kanuni ambazo zinapiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ikiwa ni njia ya kulinda mazingira.

“Tuwaombe wenzetu hasa walio katika mipaka yetu, Jeshi la Polisi na watu wa forodha kwa kuwa makini na mizigo mbalimbali inayopita katika maeneo ya mipaka ili kuzuia uingizwaji kinyemela wa mifuko ya plastiki.”

Aidha, Dk Jafo amehimiza wananchi na mamlaka za serikali za mitaa kuifanya nchi kuwa safi na kusisitiza suala la uwekaji vitunza takataka kwenye mitaa.

“Tuifanye nchi yetu iwe safi kabisa, niwaombe katika mamlaka za serikali za mitaa twende na sula zima la kuweka utamaduni wa kuweka dustbin (vihifadhia taka) kataka mitaa yetu.”

Hivi karibuni, Dk Jafo ametangaza kuanza kwa operesheni kabambe ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki inayoanza leo nchini nzima.

Katika operesheni hiyo ameagiza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushirikiana na Sekretarieti za mikoa na kutaka mkazo zaidi ufanyike kwenye masokoni, magulio, madukani na kwenye bucha za nyama na samaki hasa kutokana na watu wasiowaaminifu kugeuza vifungashio kuwa vibebeo.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rai, Dk Philip Mpango aliyeagiza mikoa yote kuanza kampeni kabambe ya kutokomeza mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na taasisi NEMC na kuhakikisha hakutoonekana tena mifuko ya plastiki katika mitaa.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button