Jaji Juma: Sijawahi kukaa na Rais, Bunge kujadili kesi

JAJI Mkuu mstaafu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema wakati wote alioshika wadhifa huo, hajawahi kukaa na rais, waziri mkuu au spika kujadili kesi hata siku moja, badala yake walikuwa wakijadili mambo yenye maslahi makubwa.

Aidha, Jaji Mkuu mpya wa Tanzania, George Masaju amesema kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kusimamia haki, maslahi ya umma na ya taifa.

Hayo yalielezwa jana katika hafla ya uapisho wa Jaji Mkuu mteule, George Masaju, iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Profesa Juma alisema ushirikiano kati ya mahakama na mihimili mingine ni ya muhimu, lakini mitandao ya kijamii imekuwa ikitoa tafsiri hasi kuwa ushirikiano huo unaingilia uhuru wa mahakama jambo ambalo si kweli.

“Hata siku moja mimi sijawahi kukaa na rais, spika au waziri mkuu tukawa tunaongelea mambo ya kesi, kwanza sina majalada hapa, siku zote tunaongelea mambo ambayo yana maslahi makubwa, kwa hiyo zile tafsiri kwamba ukionekana unafuatilia ni kuingiliwa nadhani hiyo siyo kweli,” alisema.

Alisema anachokitafuta Jaji Mkuu katika ushirikiano huo na mihimili mingine ni rasilimali za taifa ambazo zinasimamiwa na mihimili hiyo.

Pia, alimshauri Jaji Masaju kuwa ni lazima jicho lake likamate jicho la rais na kuwa aangalie anachofanya kitakavyoisaidia mahakama.

“Kama kuna sheria, kama kuna miradi, siku zote unaangalia anachokifanya kitasaidiaje mahakama na rais ni mdau muhimu sana kwa sababu bila uwekezaji wake hakuna chochote ambacho kinaweza kufanyika, kuwekeza kwenye rasilimaliwatu, anaongeza majaji, mahakimu na bajeti,” alifafanua.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za Benki ya Dunia zinapatikana.

Alisema kwa awamu ya kwanza walipata Dola za Marekani milioni 65 na mwaka 2022 aliridhia mkopo wa pili ambao ulikuwa mkubwa, lengo likiwa ni kutambua kuwa utoaji wa haki ni sehemu muhimu katika maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Jaji Masaju alisema mahakama itaendelea kusimamia kanuni zinazowaongoza ambazo ni haki, maslahi ya umma na taifa.

“Katika kutoa haki, tumepewa kanuni ambazo zinatuongoza na moja ya kanuni ni ya kutenda haki kwa watu wote bila kujali hali yake kiuchumi na kijamii na kuharakisha utoaji haki isipokuwa kama kuna sababu ya msingi, pia kutofungwa na masharti ya kiufundi yanayoweza kusaidia haki kutendeka ipasavyo,” alisema.

Katika kutekeleza maagizo ya rais ya mahakama kutoa huduma zinazolenga mwananchi wa kawaida, alisema atashauriana na wenzake namna ya kulitekeleza hilo ili kuharakisha utatuzi wa migogoro na watu kupata haki zao mapema.

“Tunaweza tukawa na mahakama ya rufaa ambayo inafanyia kazi kwa kudumu Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya haya ni mambo ambayo siwezi kusema kwa kujiamini kwa sababu ni ya kushaurina na wenzangu, lakini tukifanya hivi, uchumi utaenda haraka watu watapata haki zao kwa haraka,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Jaji Masaju ameomba  ushirikiano kutoka kwa majaji, mahakimu na watumishi wengine wa mahakama.

Akipokewa katika makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma yaliyoambatana na makabidhiano ya ofisi kati yake na Jaji mstaafu, Profesa Juma, Jaji Masaju alisema anachukia urasimu kwenye utumishi.

Masaju alisema atafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Profesa Juma. “Tuendeleze ushirikiano kama tuliokuwa nao hapo  awali, wengi  tunafahamiana, mnakaribishwa ofisini kwangu,”alisema Jaji Masaju.

Jaji Mstaafu Profesa Juma aliwasisitiza watumishi kuendelea kuharakisha usikilizaji wa kesi ili kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa kesi ambazo nyingine hukaa kwa miaka miwili.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button