Jaji Mkuu ataka wafungwa wasaidiwe kukata rufaa

Afungwa jela maisha kwa kusafirisha dawa za kulevya

JAJI Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amewataka watendaji wa mahakama kufuatilia mwenendo wa kesi za watu wanaotumikia vifungo mbalimbali ili kuwasaidia kwa ajili ya kukata rufaa kwa wale ambao hawajaridhika na hukumu zilizotolewa.

Abdalla alisema hayo wakati alipofanya ziara kutembelea magereza mbalimbali katika Kisiwa cha Pemba na kufanya mazungumzo na watendaji hao pamoja na mahakama.

Alisema kukata rufaa ni haki ya mtuhumiwa aliyehukumiwa kifungo ambaye hajaridhika na hukumu iliyotolewa mahakamani.

Advertisement

Alisema kwamba huo ni wajibu wa watendaji wa mahakama katika kuona haki inatendeka pamoja na kupunguza msongamano kwa wafungwa katika magereza yaliopo nchini.

Aidha, kwa upande wa mahakama za kadhi, Jaji Mkuu Abdalla aliwataka watendaji ikiwemo makadhi kufanya usuluhishi wa kesi zinazohusu talaka ambazo zimekuwa nyingi.

Alisema athari za talaka kwa wanandoa ni kubwa ikiwemo kusambaratika kwa familia na watoto kukosa matunzo ya baba na mama pamoja na maendeleo ya elimu.

Kwa mfano, alisema wakati mwingine makosa kwa wanandoa yanahitaji usuluhishi wa pamoja kuliko kuanza kutoa talaka ambayo athari zake ni kubwa.

”Watendaji wa mahakama ya kadhi ikiwemo mahakimu huu ni wakati wa kujipanga zaidi kuona usuluhishi wa kesi zinazohusu talaka unafanyika kwa sababu tunashuhudia wingi wa talaka ambazo matokeo yake ni kusambaratika kwa familia lakini wanawake wanaopewa talaka bado umri wao ni mdogo sana,” alisema.

Ofisa Mtendaji wa Mahakama ya Konde Pemba, Maulid Hamad Ali alisema wamejipanga kusikiliza mashauri ikiwemo ya kesi za udhalilishaji wa kijinsia kupitia mahakama maalumu ambapo mashauri yake huchukua takribani miezi mitatu kabla ya kutolewa hukumu.

”Tumeongeza kasi ya kusikiliza mashauri yanayofikishwa kwa wakati ambapo kwa sasa kesi husikilizwa na kutolewa maamuzi katika kipindi cha miezi mitatu,” alisema.

Mapema, Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Valentina Andrew Katema alisema wamejipanga kuhakikisha upelelezi wa kesi unakamilishwa kwa wakati na kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa.

”Tumejipanga kuhakikisha uchunguzi wa kesi unakamilika katika kipindi kifupi na kuanza kutajwa katika mahakama zetu, hatua ambayo itapunguza malalamiko kutoka kwa jamii kuhusu kuchelewa kusikilizwa kwa kesi,” alisema.

Jaji mkazi Pemba, Ibrahim Mzee alisema wameongeza kasi ya kusikiliza mashauri yanayofikishwa katika mahakama zilizopo Pemba zikiwemo kesi za udhalilishaji wa kijinsia.

Aidha, aliipongeza mahakama kuu kwa kuwaongezea watendaji ikiwemo mahakamu ambao kwa kiasi kikubwa wamesaidia kasi ya kusikiliza kesi na kuzitolea uamuzi kwa wakati, hatua ambayo imepunguza malalamiko kutoka kwa jamii.